Msukuma awacharukia NEMC kufungia baa, kumbi za sherehe


Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Kasheku ‘Musukuma’ ameomba mwongozo wa Spika juu kufungwa kwa kumbi na sehemu za starehe kwa kigezo cha kuzidisha sauti huku akisisitiza kuwa hatua hiyo imeleta taharuki katika jamii.


Akitumia Kanuni ya 76, Musukuma ameomba mwongozo wa Spika leo asubuhi jijini Dodoma akisema kuwa wananchi wengi hufanya kazi muda wote wa juma isipokuwa mwisho wa wiki ambapo huzitumia siku hizo hujiburudisha lakini kwa sasa maeneo ya starehe zikiwemo klabu katika majiji ya Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam zimefungwa.

Takribani siku saba zilizopita, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Samuel Gwamaka alitangaza kuwa jumla ya baa na kumbi za starehe 89 zimefungiwa baada ya kubainika kuwa kupiga kelele na mitetemo iliyozidi viwango vinavyotakiwa.

Hata hivyo, mbunge huyo machachari anapingana na hilo kwa kusema kusema kuwa mbali na maeneo hayo kutumika kuondoa msongo wa mawazo kwa wananchi, serikali inaingiza mapato hivyo kufungwa kwa kigezo cha kelele serikali inakosa makusanyo yake.

Amekwenda mbali na kulifananisha suala hilo na mgomo unaoendelea Kariakoo ambao umeibuliwa na Mbunge wa Makete, Festo Sanga mapema leo bungeni.

Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo, Spika Tulia Ackson amesema Kanuni ya 76 inahusu jambo lililotokea Bungeni.

“Kwa hoja aliyoileta Musukuma, jambo hilo halipo katika kanuni hiyo ya Mwongozo,” alisema Dk Tulia.

Hata hivyo Spika amelieleza Bunge kuwa mbunge huyo anaweza kuwasilisha hoja hiyo kupitia kanuni nyingine ikiwa anaona inafaa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo