Mkurugenzi awanunulia sare wanafunzi wa Kidato cha Kwanza

Mkurugenzi wa Halmashuri ya wilaya ya Kishapu Emmanuel Johson akitoa fedha kwa Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Isoso ili akanunue Sare za Sekondari.


Na Marco Maduhu, KISHAPU

MKURUGENZI wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Emmanuel Johnson, amesema katika halmashauri hiyo wanafunzi wote ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanapaswa kuripoti shuleni bila kujali hawana Sare za Sekondari bali waende hata na Sare za Shule ya Msingi, ili wakaanze masomo wakati taratibu zingine zikiendelea za kununuliwa Sare za Sekondari.

Johnson amebainisha hayo leo Marchi 2, 2023 wakati alipotembelea Shule ya Sekondari Isoso wilayani humo kuona mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na kukuta mahudhurio ni mazuri, ambapo wamesalia wanafunzi wawili tu ambao ndiyo hawajaripoti shule, huku wengine wakiwa darasani na Sare za shule ya Msingi.

Amesema katika Halmashauri hiyo ya wilaya ya Kishapu hadi sasa wamefikisha asilimia 98.17 ya wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao wamesharipoti shule, na kuagiza wale ambao wamesali hadi kufikia Marchi 29 mwaka huu, wawe wamesharipoti shule hata kama hawana Sare za Sekondari bali wavae za Shule ya Msingi ili wasiendelee kukosa masomo.

“Natoa wito kwa wazazi wapeleke watoto wao shule ambao wamefaulu kujiunga na kidato cha kwanza hata kama hawana Sare za Sekondari bali wavae za Shule ya Msingi, ili waendelee na masomo, na sisi Halmashauri tutaona namna ya kuwasaidia kwa kuwanunulia Sare ili wafanane na wenzao,”amesema Johnson.

“Leo nimetembelea hapa Shule ya Sekondari Isoso na nimekuta wanafunzi wawili wa kidato cha kwanza wakiendelea na masomo yao huku wakiwa wamevaa Sare za Shule ya Msingi nimependa ujasiri wao wakupenda masomo, na mimi nimetoa fedha ili wakanunue Sare za Sekondari na kufanana na wenzao, na nitafanya hivyo kwa shule zote ambazo nitakuta wanafunzi hawana Sare za Sekondari,” ameongeza.

Aidha, amesema pia hali ya uandikishaji watoto darasa la awali wamefikisha asilimia 101, na uandikishaji darasa la kwanza wamefikisha asilimia 108, kidato cha kwanza asilimia 98.17.

Naye Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya wilaya ya Kishapu David Mashauri, amesema kwa wanafunzi ambao wamesalia kuripoti shule wa kidato cha kwanza watawasaka wote kwa kushirikiana na viongozi wa vitongoji, vijiji na Kata ili waanze masomo mara moja na kuungana na wenzao.

Nao wanafunzi ambao wamekutwa wakisoma na Sare za Shule ya Msingi, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga miundombinu ya shule ili wapate elimu katika mazingira Rafiki, pamoja na Mkurugenzi wa Kishapu Emmanuel Johnson kutoa pesa na kuwanunulia Sare za Shule ya Sekondari na kuahidi watasoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo