Kijana Magilu Ilinga (23) mkazi wa Kijiji cha Nduha Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza ameuawa kwa kipigo cha wananchi wenye hasira kali waliochukizwa na kitendo chake cha kumuuwa kikongwe, Elizabeth Lingitela (76).
Ofisa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza, Leonard Nyaoga aliyefika kijijini hapo kuwapa pole familia ya Elizabeth amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akiitaka jamii kutambua na kudhibiti vitendo vya kihalifu zinaeleza kuwa vifo vya wawili hao vilitokea Jumapili Februari 26, mwaka huu.
Akizungumza wakati wa mkutano wa elimu kwa jamii kijijini hapo, jana Jumatano, Machi 1, 2023, Ofisa Mtendeji Kijiji Cha Nduha, James Makelemo amesema Magilu aliuawa kwa kushambuliwa na wananchi muda mfupi baada ya kushikiliwa kwa tuhuma za kumuuwa kwa kumkata panga kikongwe Elizabeth kwa kile kinachodaiwa ni imani za kishirikina.
“Bibi Elizabeth aliuawa mchana wa Jumapili Februari 26, 2023 katika tukio lililotokea Kitongoji cha mwabuchuma. Nilipigiwa simu na kufika eneo la tukio na kumkuta mtuhumiwa akiwa tayari amekamatwa,” amesema Ofisa Mtendaji huyo
Amesema kutokana na taharuki na hamaki iliyokuwepo, alilazimika kujitenga pembeni kidogo kwa lengo la kupiga simu kuomba nguvu kutoka Jeshi la Polisi ili kumfikisha mtuhumiwa kituoni kwa hatua za sheria; lakini ghafla wananchi walianza kumshambulia kwa kipigo mtuhumiwa huyo hadi kufa.
“Kipigo kile kilisababisha kifo cha mtuhumiwa pale pale,” amesema Mekelemo.
Chanzo: Mwananchi