Mamake marehemu Steven Charles Kanumba Flora Mutegoa amemlaani vikali mhubiri wa kike Mfalme Zumaridi dhidi ya madai kuwa atamfufua mwigizaji huyo aliyeaga dunia.
Mtanzania huyo alifariki dunia miaka 12 iliyopita na alisifika kwa uhusika wake mkuu katika filamu mbalimbali na pia alikuwa mtayarishaji na mwandishi wa hadithi. “Ukiona Kanumba anatembea, usishtuke nimekimbilia kwenye vyombo vya habari kusema hivyo,” aliwaambia waumini wa kanisa hilo waliokuwa wamejawa na jazba na kurukaruka kwa furaha wakitarajia kumuona mwigizaji huyo kipenzi.
Video ilipotoka nje, Flora aliipata na ilimuathiri sana. Katika mahojiano na Global TV Online, mwigizaji huyo ambaye alitokwa na machozi alisema hata manabii waliokuwa na imani kubwa kwa Mungu hawakufufuka kwa hiyo Kanumba atarudi vipi?
"Unataka kumfufua Kanumba ili uwe naye? Naomba nipe mwanangu ikiwa unaye," alisema. "Sitamfanyia lolote ila nitamwachia Mungu aliye hai," aliongeza. Flora alisimulia kuwa mhubiri huyo aliwahi kumpeleka kwa ndege hadi kwenye kanisa lake na alikuwa akimlazimisha kuwaambia vyombo vya habari kuwa alimuona marehemu muigizaji katika ndoto zake sawa na muumini mmoja wa kanisa hilo.
"Aliniita nyumbani kwake miaka saba iliyopita akisema alikuwa akimtokea kwenye ndoto na nikamwambia kuwa akikutokea nyie basi anakupenda, simuoni. Nikamwambia siwezi kwenda kinyume na Mungu ili kumpendeza,” alisema Flora ambaye ni Mkristo aliyeokoka. "Kama anaweza kufufua watu, ana ndugu wangapi na hata babake pia aliaga dunia, kwa nini hawezi basi kuwafufua?" aliema Flora kwa hasira.
Flora aliongeza kuwa iwapo Zumadiri alitaka kumfufua mtu hivyo basi anaweza kuanza na marehemu John Pombe Maghufuli aliyekuwa rais wa nchi hiyo ambaye alipendwa na watu wote na hata habari za kifo chake zilimfanya azirai. "Tafuta kiki ingine usitafute kiki na mwanangu mi naumia, mimi ndio mamake. Waliibuka Kanumba ni Freemason nikakaa kimya na huyu anaibuka na hili," alikumbuka kwa masikitiko.