Watu tisa wanaosadikiwa kuwa majambazi, wakiwa na silaha za moto na za jadi, wamevamia na kuteka magari 10, likiwamo lililokuwa limebeba maiti ya mwanafunzi na kisha kuwapora fedha, simu na vitu vingine mbalimbali abiria waliokuwa wakisafiria magari hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa saba usiku wa Februari 17 mwaka huu kwenye Msitu wa Nyimbili, Kata ya Mtungwa wilayani Momba mkoani Songwe, barabara kuu ya Mlowo-Kamsamba.
Alisema washukiwa hao waliokuwa na bunduki, mapanga na mashoka, waliwaamuru abiria kwenye magari kushuka kisha kuwapora mali zao.
Alisema kati ya magari 10 yaliyotekwa kwenye msitu huo ambao ni maarufu kwa jina la Msitu wa BoT, moja lilikuwa limebeba maiti ya mwanafunzi lenye namba za usajili SM 14056 lililokuwa linasafiri kutoka wilayani Momba kwenda wilayani Mbozi.
Kamanda Mallya alisema watuhumiwa hao baada ya kuteka magari hayo, waliwapora abiria simu na fedha, akibainisha kuwa kwenye gari lililobeba maiti, walipora fedha taslimu Sh. 216,000 pamoja na simu za watu waliokuwa wakisindikiza maiti hiyo zenye thamani ya Sh. 1,200,000.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo kutokea, polisi walianza msako haraka na kufanikiwa kuwakamata watu sita wanaosadikiwa kuhusika katika tukio hilo na mmoja wa watuhumiwa alikutwa na simu mbili ambazo zinasadikiwa kuporwa eneo la tukio.
Kamanda Mallya aliwataja waliokamatwa kuwa ni Shughuli Siame (47), mkazi wa Kijiji cha Nambinzo; Furaha Sembuli (49), mkazi wa Mlowo wilayani Mbozi na Andalwisye Gwalamba (41), mkazi wa Kijiji cha Ntungwa Wilaya ya Momba.
Wengine ni Oden Simtenda (45), mkazi wa Ntungwa; Lowa Simbeye (51), mkazi wa Ntungwa na Andrew Simlembe, mkazi wa Kijiji cha Chilulumo wilayani Momba.
Kamanda Mallya alisema kufuatia mfululizo wa matukio ya ujambazi eneo hilo, Jeshi la Polisi limeweka utaratibu wa kuimarisha ulinzi eneo la msitu huo saa 24.
Ndani ya mwezi mmoja na nusu, watuhumiwa wa ujambazi wamefanya uporaji kwenye msitu huo mara mbili, tukio la juzi likiwa la tatu ndani ya kipindi hicho kifupi.
Katika tukio la kwanza, waliteka magari manne majira ya saa nne usiku yaliyokuwa yakitokea mnadani kijijini Kamsamba na tukio la pili waliteka basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster na Noah.