Kila kuchao ‘watumishi’ wa Mungu wanazidi kuibuka na visanga vya kila aina kupitia vituko wanavyowatendea waumini wao.
Wahubiri wa karne ya sasa wanapenda sana utata kuliko kuelekeza juhudi zao kueneza mafunzo ya Biblia.
Yote tisa huko mtaani Githurai, katika kaunti ya Kiambu, tulipatana na pasta John Mwangi ambaye hawezi kukanyaga chini akisema imejaa dhambi hivyo hubebwa na kondoo wake.
Mwangi, anaamini kuwa yeye ni mchungaji aliye karibu sana na Mungu, kwa hivyo hawezi kutembea kwenye ardhi yenye dhambi.
Akieleza sababu za ardhi kuwa yenye dhambi, anamaanisha kuwa wakati damu ya watu wasio na hatia inapomwagika chini inafanya ardhi kuwa na dhambi zaidi.
Ikumbukwe pia kuwa, Mchungaji mmoja kutoka nchini Nigeria alizua mjadala katika mitandao kijamii siku ya wikendi baada ya kubeba bunduki kanisani alipokuwa akihubiri.
Pasta Uche Aigbe mwandamizi wa Kanisa la House on the Rock mjini Abuja, alizua tafrani wakati wa Ibada ya Jumapili, Februari 12, alipopanda kwenye mimbari akiwa amebeba bunduki aina ya AK-47.