Waandishi wa habari wameshirikiana na majirani katika maandalizi na taratibu za kuaga mwili wa aliyekuwa msichana wa kazi za ndani Aneth Kassim (17) na kisha mwili wake kusafirishwa leo kuelekea Ngara kwa maziko.
Kaka wa binti huyo, Imani Benjamin ndiye ndugu pekee aliyefuata mwili akitokea Kijiji cha Mkikomelo, Kata ya Mgoma, Wilaya ya Ngara hali iliyowafanya waandishi wa habari kushiriki zoezi hilo kwa kushirikiana na majirani waliojitokeza.
Mwili wa Aneth umesafirishwa leo Jumamosi mchana kwa gari kuelekea Ngara na unatarajiwa kuzikwa siku ya Jumatatu kijijini kwao Mkokomelo.
Aneth ambaye alizaliwa mwaka 2005, alifikwa na umauti Februari 8 akiwa na mwajiri wake Diana Joseph anayetuhumiwa kumuua Anneth majira ya saa mbili usiku nyumbani kwake na kumfikisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akidai alimkuta binti huyo amejinyonga bafuni.