Masomo yalisitishwa katika Chuo cha Kiufundi cha Lamu jana Jumatatu, baada wanafunzi kuzua fujo iliyodaiwa kuchochewa na majini.
Mkanganyiko ulianza mwendo wa saa nne asubuhi wakati mwanafunzi wa kike alianza kupiga kelele na kutamka maneno yasiyoeleweka.
Walioshuhudia, walisema jitihada za kumdhibiti hazikufua dafu kwani alianza kuwashambulia walimu na wanafunzi kwa ngumi na makofi.
Wanafunzi wengine watano nao walianza kutenda vivyo hivyo, wakiingia katika baadhi ya madarasa na kuwapiga wenzao.
Mkurugenzi wa chuo hicho, Bw Fidel Mulei, hata hivyo alipuuzilia mbali madai kuhusu majini akisema mwanafunzi aliyeanza kelele alikuwa amekasirishwa na wenzake.
Alisema waliamua kufunga chuo wakati wengine pia walianza fujo, lakini walitarajiwa kurudi baadaye.
Mhubiri wa Kiislamu, Bw Mahmoud Ahmed Abdulkadir, alisema tabia hizo huchochewa na saikolojia hasa baina ya wanawake, lakini huwa wanarudia hali ya kawaida baada ya muda mfupi.