Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro, linamshikilia, August Matemu, Mkazi wa Kirua Vunjo, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro kwa mauaji ya mkewe, Fausta Tesha(26) na mtoto mchanga wa wiki mbili aitwaye Rodrigo Mgaya chanzo kikielezwa ni wivu wa mapenzi.
Febrauri 22, mwaka huu mwanaume huyo alimvizia mkewe akiwa amelala usiku na mtoto wake mchanga wa wiki mbili na kuwachoma visu sehemu mbalimbali za miili yao ambapo mwanamke huyo alifariki papo hapo huku kichanga kilichojeruhiwa sehemu ya tumboni na kisu na kisha utumbo kutoka nje akifariki Februari 25 mwaka huu katika hospitali ya KCMC.
Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa Februari 27 katika kijiji cha Marua, Kirua Vunjo Mashariki akiwa amelala kichakani hajitambui kwa kukosa chakula.
"Huyu mtuhumiwa baada ya kutekeleza mauaji haya Febrauri 22 katika kijiji cha Mero, alikimbia ambapo mwanamke aitwaye Fausta Tesha alijeruhiwa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali, maeneo ya kifuani, ubavuni na tumboni pamoja na kujeruhi mtoto wa wiki mbili maeneo ya tumboni ambaye alifariki Februari 25 akipatiwa matibabu KCMC, "
Aidha, Kamanda Maigwa amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Chanzo:Mwananchidigital