Wananchi wa mtaa wa Nyanza, kata ya Kalangalala iliyopo halmashauri ya mji Geita wameiomba serikali kumtoa madarakani mwenyekiti wa mtaa huo Sijaona Selemani ambaye ana tuhuma za ubadhilifu wa shilingi milioni 300 na kushindwa kusoma mapato na matumizi kwa wananchi kwa muda wa miaka mitatu
Baadhi ya wananchi wakiongea kwenye mkutano wa hadhara wamemtaka mwenyekiti huyo aachie madaraka ili uchunguzi uweze kubaini fedha hizo zilienda wapi.
"Kuna mpiga kiporomondo ambae kwa mwaka tunapiga mara nne tunamlipa shilingi 20,000/= lakini wao kwenye karatasi wameandika 1,500,000/=, hivyo ni vitu ambavyo haviingii akilini, haya ukiangalia hili jengo ambalo ni ofisi linatuambia milioni 34, wakati haina msingi wa mawe ni block tu kuanzia chini mpaka juu", alisema Mathias.
"Hivi anaechunguza huyu, atachunguzaje mtu yupo madarakani, inawezekanikaje kumchunguza mtu yupo madarakani, mtendaji naomba mwenyekiti leo hicho kiti akiachie tutafute hata mwenyekiti wa chama akae hapo akaimu", alisema Ruchagura.
"Mtu ambae tunamlenga hapa ni mwenyekiti kutumia ofisi vibaya", alisema Kasebele.
Mtendaji wa kata ya kalangalala Hamad Hussein amewataka wachi kuwa watulivu kusubiri ripoti ya mkaguzi wa ndani
"Naomba mniruhusu, nimruhusu mwenyekiti aahirishe kikao, mkaguzi wa ndani yani afanye ukaguzi wa kina tuone matatizo na mapungufu yaliyopo, mimi kama mtendaji wa kata sina mamlaka ya kumtoa mwenyekiti bado napenda kazi yangu, lakini swala la mapato na matumizi Nyanza ni sugu sio huyu peke yake hapa", alisema Hussein.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo Sijaona Selemani amejibu tuhuma hizo na kueleza kuhusu tuhuma anazotuhumiwa nazo
"Pesa hii haipo milioni 300, mheshimiwa mwandishi wa habari hii pesa haipo maana yake ni 60,000/=, kwa kila kijana nina vijana 48, kwahiyo milioni 300, yani inakuwa ni kitu ambacho kinanishangaza na kunisikitisha lakini kwa vile kuna wakaguzi wa ndani ambao wamekuja wanafanya hesabu hiyo na ukaguzi wa ndani labda tuwasubirie watakapotoa Tathmini ya namna gani madai yalivyo", alisema Selemani.