Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limethibitisha kifo cha Abdiel Raphael (42) mkazi wa eneo la Nyankumbu Mjini Geita Mkoani Geita Mchungaji wa kujitegemea ambaye amefariki baada ya kufunga kwa maombi ya siku nane bila kula huku akiwaaminisha waamini wake wasifanye chochote kwani baada ya kifo atafufuka.
Akizungumzia tukio hilo, Leo Desemba 15, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Safia Jongo amesema mchungaji huyo alikuwa na kanisa nyumbani kwake na wakati anaingia kwenye maombi hayo aliwaambia waamini wake hata wakiwa wanamuita asipoitika wasiwe na wasiwasi kwani atafufuka siku ya nane.
"Mkewe na waamini waligundua tarehe 3 disemba 2022 kuwa Mchungaji ameshafariki Ila Kwa sababu aliwaambia mwanzo hata wakimuita asipoitika wasiwe na wasiwasi, hawakutoa taarifa.
"Siku zilivyozidi kwenda mpaka tarehe 8 wakaona hafafuki ndipo tarehe 9 disemba 2022 wakaamua watoe taarifa ya kifo cha mchungaji wao" Ameeleza Jongo.
"Uchunguzi ulivyofanyika ulibaini kuwa mchungaji huyo alifariki kwa sababu ya kutokula kwa mda mrefu maana alikaa siku nane bila kula chochote.”