WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakabidhi kwa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Muhasibu wa Chuo cha Ualimu Sumbawanga, Eric Rutyamirwa na Mkufunzi wa chuo hicho Godfrey Msenuka kwa tuhuma za kuchoma nyaraka za Serikali na hivyo kupoteza taarifa za mradi wa ujenzi wa chuo cha Ualimu Sumbawanga.
Rutyamirwa na Msenuka ambaye alikuwa katibu wa ujenzi wanadaiwa kuchoma nyaraka hizo na hivyo kupoteza kumbukumbu za ujenzi wa mradi huo ambao manunuzi ya vifaa vya ujenzi yanadaiwa kufanywa mara tatu zaidi ya gharama halisi.
Mheshimiwa Majaliwa amewakabidhi watendaji kwa TAKUKURU jana (Alhamisi, Desemba 15, 2022) baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaojengwa katika kijiji cha Pito Sumbawanga mkoani Rukwa.
Ujenzi wa mradi huo unaojengwa kwa awamu mbili unatarajiwa kugharimu sh bilioni 7.1 na tayari Serikali imeshatoa shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya awamu ya kwanza. Mradi huo ulianza Agosti 2021 na unatarajiwa kukamilika Januari 2023.
Waziri Mkuu alisema baada ya kubaini kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za mradi huo na wizara husika kupanga kwenda kufanya uchunguzi ofisi ya muhasibu ambayo ndio ilikuwa na nyaraka iliungua. "Nyaraka ziliungua ndani ya ofisi ya Muhasibu huku chanzo cha moto bado hakijajulikana lakini mfumo wa umeme haukuwa na hitilafu ulikuwa salama hata baada ya tukio la moto kutokea"
Aidha, Waziri Mkuu alihoji ni kwanini mhasibu wa chuo hicho alijipa kazi ya kutunza nyaraka za ujenzi wa chuo hicho kinyume na taratibu kwa sababu aliyepaswa kuwa na nyaraka hizo ni Katibu wa Kamati ya ujenzi, hivyo aliagiza wote wachunguzwe.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga alitangaza kuivunja kamati ya ujenzi ili kupisha uchunguzi na kuunda kamati mpya ambayo itasimamia ujenzi hadi pale utakapokamilika.