Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 22 Mkazi wa Maganzo Wilaya Kishapu Mkoani Shinyanga amebakwa na mtu asiyefahamika kabla alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali kisha kumvutia kichakani na kumfanyia ukatili huo.
Tukio hilo la ubakaji limetokea Desemba 26, Mwaka huu majira ya saa 12 katika kijiji cha Bulumbaga Kata ya Maganzo Wilayani Kishapu Mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari mwanamke huyo amesema majira ya saa 12 alikuwa akielekea kazini ndipo alipokutana na mwanaume huyo ambaye alimsalimia na kumwambia ana elfu tatu anataka afanye nae mapenzi ambapo mwanamke huyo alikataa ndipo mtuhumiwa huyo alimpiga na kumvutia kichakani kisha kumfanyia kitendo hicho.
"Nilikuwa nikielekea kazini, nikakutana na kijana akadai anipe hela nifanye naye mapenzi ndipo nikakataa kupokea hela nilivyokataa akanipiga alafu akanivutia sehemu ambako hamna watu alafu akaanza kunibaka na kunitishia kuniua, aliyenisaidia ndiyo aliyetoa taarifa kituoni, Naliomba Jeshi la Polisi kuchukua hatua kiaheria kwa mtu huyo" amesema Muhanga huyo.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga, Dr.John Luzila, amethibitisha kumpokea muhanga huyo akiwa amejeruhiwa na kitu chenye makali katika mwili wake ambapo walimpatia huduma ya kwanza na hadi kufikia saivi hali yake ni nzuri.
Aidha Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Shinyanga, ACP Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amebainisha kuwa mwanamke huyo alibakwa na kijana mwenye umri wa miaka 23, Masanja Johakim Mkazi wa Maganzo huku akitoa wito kwa wananchi wote kutoa taarifa za matukio ya ukatili ili kukomesha uovu huo.
"Tunafahamu kuhusu tukio hilo ambalo lilitokea Desemba 26 Kata ya Maganzo, kulingana na maelezo aliyotoa muhanga alisema kuwa alibakwa na mtu ambaye anajulikana kwa kina la Masanja Johakim ambapo alimchoma na kitu chenye ncha kali kabla ya kumfanyia unyama huo, sisi kama Polisi kutasimama imara na tutafanya uchunguzi kwa kina juu ya tukio hili" amesema Magomi.