Watu wawili wamenusurika kifo huku wasadikiwa kivunjika miguu katika ajali iliyohusisha gari ya Toyota RAV4 yenye usajili namba T 156 BDX na pikipiki yenye usajili namba MC 144 DFF iliyotokea eneo la Mkuyuni sokoni jijini Mwanza majira ya saa moja na robo usiku chanzo kikielezwa kuwa ni mwendo kasi
Akisimulia tukio hilo Sharifu Shabani shuhuda ameieleza Nipashe kuwa chanzo cha ajili hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa gari ambaye alichepuka kuvuka mstari mweupe bila kuchukua taadhari akielekea mkono wake wa kulia kwaajili ya kupisha gari la abiria lilokuwa likielekea katika kituo cha daladala Mkuyuni.
Shabani amesema, baada ya dereva kuchepuka kwa ghafla kwa kasi ndipo alipokuta na kumgonga mwendesha pikipiki aliyekuwa amebeba abilia mmoja na wote kuvunjwa miguu yao ya upande wa kulia.
Watu hao waliojulikana awali kwa jina moja ambapo dereva wa pikipiki alijulika kwa jina la Thomas anayefanya shughuli za kusamba kreti za bia huku aliyekuwa amebebwa na pikipiki alijulika Bahati.
Baada ya kutokea kwa ajali hiyo askari wa usalama barabarani walifika haraka na kuita gari la wagonjwa lililowapeleka majeruhi hao hospitalini kwaajili ya matibabu zaidi.


