Shemeji matatani kwa kumpa mimba mhitimu wa darasa la 7

MHITIMU wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Lemosho iliyoko Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, ambaye anasubiri kutangazwa kwa matokeo ya mitihani ya taifa, amepata ujauzito baada ya kudanganywa na shemeji yake kwamba akifanya naye mapenzi atapona ugonjwa wa kutokwa damu unaomsumbua.


Msichana huyo (jina limehifadhiwa), baada ya kuhojiwa na kufanyiwa vipimo vya kitabibu katika Hospitali ya Wilaya hiyo, amegundulika kuwa na ujauzito wa miezi sita.


Jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matadi, Asanterabi Ng'onda, akizungumzia tukio hilo, alikiri ni kweli msichana huyo amepata ujauzito na mtuhumiwa aliyetajwa na mtoto huyo ni shemeji yake.


“Ni kweli ofisi yangu imepokea taarifa hiyo kutoka kwa ndugu wa msichana, kwamba binti yao amepewa ujauzito na shemeji yake. Jambo hilo kwangu mimi kama mzazi limenisikitisha sana.


“Mtoto anasubiri matokeo ili ajiunge na kidato cha kwanza, lakini mtu anadiriki kufanya mapenzi na mtoto mdogo. Hii haipendezi kwenye jamii, tumeanza kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia ili kudhibiti wimbi la matukio haya,” alisema.


Inaelezwa kuwa msichana huyo alipata ujauzito huo katikati ya mwaka huu, wakati akipewa dawa ya kuzuia kutokwa na damu puani na sehemu za siri.


Akizungumza na timu ya wanaharakati wa haki za binadamu wanaofuatilia tukio hilo, ndugu wa msichana huyo alisema: "Shemeji alimwambia ili kizazi kisioze kutokana na kutoka damu sehemu za siri ni lazima afanye naye mapenzi ili dawa ifanye kazi. Sasa sisi hatujui kama ni mganga wa kienyeji alimwelekeza hivyo au ni shemeji tu tamaa zake hatujui.”


Alisema kabla ya msichana huyo kupata ujauzito, shemeji yao aitwaye Abed Salim, ndiye aliyekuwa akishughulikia tatizo la mtoto huyo ili apone maradhi yanayomsumbua na kurejea shuleni kuendelea na masomo yake.


“Tulimpa kazi ya kumshughulikia msichana huyo kwa sababu tatizo lake lilikuwa la mara kwa mara. Aliondoka naye Lemosho na kwenda kwa mganga wa kienyeji huko mkoani Tanga ili kutafuta tiba na alifanikiwa hadi huyo mtoto akapona.


“Lakini cha kushangaza, baada ya muda tumemkuta mdogo wetu ana ujauzito, wakati bado anasubiri matokeo ya darasa la saba. Ikabidi tumhoji ni nani amempatia ujauzito huo, alikuwa hataki kusema, tukambana na akamtaja shemeji yake kwamba ndiyo aliyempa ujauzito na akasema aliupata wakati shemeji akimpa dawa za kuzuia damu kutoka puani na sehemu za siri,” alisema.


Mratibu wa Kukuza Usawa kwa Elimu ya Haki za Binadamu wa Shirika la Maendeleo la TUSONGE CDO linalotekeleza mradi huo katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, Consolatha Kinabo, alisema licha ya kazi kubwa inayofanywa ya kubomoa mawazo mgando ya jamii na kupaza sauti kukemea vitendo hivyo, bado nguvu zaidi zinahitajika kupambana na ongezeko la matukio ya ulawiti, ubakaji na unajisi katika Wilaya ya Siha, kwa kuwa ni eneo tishio la ukatili.


Kinabo alisema tayari wamependekeza kwa serikali za vijiji na kata, kila wakati kutolewe elimu ya sheria na madhara ya ukatili wa kingono kwa wanawake na watoto pamoja na kurejewa taratibu za kimila zinazokinzana na misingi ya haki za binadamu.

Chanzo:Nipashe


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo