Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amewaasa Watanzania kupunguza na kuacha kabisa kutenda dhambi na badala yake wamrudie Mwenyezi Mungu ili kuwaepusha na adha ya ukame ulioikumba nchi.
Amesema kukosekana kwa mvua, uwepo wa ukame na kukauka kwa maji ardhini ni ishara kwamba watu wanatenda maasi.
Hata hivyo mabadiliko ya tabianchi yanatajwa kuwa ni sababu ya ongezeko la joto, mvua zisizotabirika pamoja na ukame.
Mufti ameyasema hayo leo Jumamosi Novemba 5, 2022 alipokuwa akiongoza dua maalum ya maadhimisho ya miaka 26 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).
“Tunapoomba mvua tuendelee kuacha maasi na mambo mengine yasiyofaa, watu waache dhuluma, mambo mabaya yanayosababisha sisi Mwenyezi Mungu atunyime mvua,” amesema Mufti Zuberi.