Ndege ya abiria imeanguka katika eneo la Ziwa Victoria mkoani Kagera.
Ndege hiyo imeanguka leo asubuhi mjini Bukoba.
Polisi wamethibitisha kutokea kwa ajali hiyo. Askari wa zimamoto na uokoaji pamoja na polisi na wavuvi wa eneo hilo wako kwenye eneo la tukio wakifanya shughuli ya uokoaji.
Shirika la Ndege la Precision limethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyohusisha ndege namba PW 494 kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba.
Shirika hilo limesema ndege hiyo ilipata ajali ilipokuwa ikikaribia uwanja wa ndege wa Bukoba.
Limesema kuwa timu ya uokoaji imekwenda eneo la tukio na taarifa zaidi zitatolewa saa mbili zijazo.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kutokana na mkasa huo.
"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya ndege ya Shirika la Precision katika Ziwa Victoria, mkoani Kagera. Natuma salamu za pole kwa wote walioathirika na ajali hii. Tuendelee kuwa watulivu wakati huu zoezi la uokoaji likiendelea huku tukimuomba Mwenyezi Mungu atusaidie."