BARAZA la mawaziri limeagiza wataalamu wa ndani na nje ya nchi washirikiane kufanya uchunguzi wa kujua chanzo cha ajali ya ndege ya Precision Air aina ya ATR42-500 yenye namba ya usajili PW494.
Ajali hiyo ilitokea Novemba 06, mwaka huu na ilisababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 26 baada ya ndege hiyo kutumbukia kwenye Ziwa Victoria wakati ikitaka kutua uwanja wa Bukoba.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma mara baada ya Baraza hilo lililoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kumaliza kikao chake, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema wataalamu watafanya uchunguzi wa chanzo cha ajali na kushauri hatua za kuchukua.
Amesema taarifa ya awali itatolewa kwa siku 14 kuanzia siku ya ajali, taarifa ya pili itatolewa baada ya siku 30 na nyingine itakuwa ndani ya miezi 12.