UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umemjia juu mbunge wa kuteuliwa, Dk. Bashiru Ali na kumtaka kuomba radhi kutokana na kauli yake aliyoitoa hivi karibuni ya kuonyesha kukerwa na wanaosifia utawala kwa kutumia maneno ‘anaupiga mwingi’.
Dk. Bashiru ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, juzi akiwa kwenye mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoani Morogoro, alinukuliwa akisema maneno mbalimbali yaliyotafsiriwa na umoja huo kuwa yana ukakasi kwa kuwa yametolewa na aliyekuwa kiongozi wa chama hicho na hakusita kupongeza serikali kwa wakati huo.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi, alisema: "Amezungumza maneno ambayo si rafiki, si ya kiungwana, yamejaa ukakasi na yamelenga kuchonganisha serikali na wananchi, hasa wakulima.
“Sisi UVCCM hatukubaliani na jambo hilo na serikali ya awamu ya sita inafanya kazi kubwa ambayo inakwenda kuacha alama katika eneo la wakulima.
"Katika suala hilo tunaweza kutizama kipindi hicho bei ya mbolea ilipanda bei sana na ongezeko lile lilipelekea Rais Samia Suluhu Hassan (serikali) kutoa ruzuku ya Sh. bilioni 150 ili kupunguza bei ambayo ilikuwa Sh. 130,000 na kuendelea."
Kihongosi alisema serikali imeweka utaratibu wa wakulima kununua mbolea kwa bei nafuu, jambo ambalo limegusa maisha yao na uchumi wa nchi.
"Sasa anapotokea kiongozi ambaye alikuwa na dhamana kubwa anatoa maneno yenye ukakasi kwamba viongozi hawapaswi kupongezwa, bali wanapaswa kutolewa matamko ya kuwashinikiza, hii sio sawa, nitoe rai kwa viongozi, tabia hii sio njema.
"Lakini ikumbukwe serikali imetoa vitendea kazi kwa maofisa ugani nchi nzima, zaidi ya 6,000 na vipima udongo, serikali imeweka fedha pale kusaidia kukuza uchumi hasa sekta ya kilimo, kwa sababu watazalisha kwa kiwango kingi kuuzwa ndani na nje ya taifa letu.
"Sasa inapotokea mtu kubeza jitihada za serikali. Tunamtaka kiongozi Dk. Bashiru kujitizama na kujitathmini hiki anachopanda kina faida gani kwa taifa letu?" Kihongosi alisema.
Alifafanua kuwa Dk. Bashiru ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kilimo na anajua kila kilichofanyika kwenye sekta hiyo na namna bajeti ilivyoongezeka katika mwaka huu wa fedha, hivyo anapofikia kutoa kauli hiyo ni jambo la kushangaza.
"Tujikumbushe ndugu Bashiru akiwa kiongozi mara nyingi ametoa pongezi kwa serikali na amekuwa akipongeza kwa kazi nzuri na njema iliyokuwa inafanywa na serikali sasa heshima aliyoitumia kipindi kilichopita, heshima ileile aitumie kwa kipindi hiki kwa sababu serikali bado ni moja na chama bado ni kilekile, wajibu wake ni kuwa na utii kwa mamlaka ambayo ipo madarakani," alisema.
Nipashe ilimtafuta Dk. Bashiru kuzungumzia suala hilo, lakini simu yake iliita pasina kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi ili kutoa ufafanuzi, hakujibu.
Chanzo:Gazeti Nipashe
