Mwanafunzi wa Kidato cha tatu shule ya Sekondari ya Nyabubela iliyopo kata ya Kasamwa mjini Geita ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nyakahongola anayefahamika kwa jina la Janet Charles (18) amefariki dunia kwa kunywa sumu ya panya huku chanzo kikiwa hakijafahamika.
Akizungumzia tukio hilo wakati wa mazishi ya mwanafunzi huyo nyumbani kwao Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Nyakahongola, Paul Mgini amesema Janeth alipokelewa zahanati akiwa na hali mbaya na kuanza kupatiwa matatibabu ya awali kuokoa uhai wake.
"kadri mda ulivyozidi kwenda, hali ya Janeth ilikuwa inazidi kuwa mbaya, badaye akasema kuwa amekunywa sumu ya panya lakini hakusema chanzo ni nini baada ya dakika 10 akapoteza maisha" Amesema Paul.
Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Nyakahongola, Rubigisa Boazi amekiri kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo na kuomba Wazazi na walezi wawe wa kwanza kuwatia moyo watoto pindi wanapopitia magumu.