
TANESCO imerudisha tozo ya huduma kwa wateja wake wanaotumia umeme kwa matumizi ya nyumbani ambao walikuwa wameondolewa kwa muda mrefu ambapo sasa inamlazimu mteja wa TANESCO kila mwezi kukatwa tozo ya huduma ‘Service charge’ ambayo ni shilingi 6740.
Kwa kawaida kiasi hicho cha fedha kinakatwa kwanza ndipo mteja anaporuhusiwa kununua umeme kulingana na mahitaji yake. Kwa mujibu wa TANESCO mteja analipia tozo ya huduma kila mwezi bila kujali iwapo ametumia umeme au la (analipia sh. 5520). Kiasi hicho cha fedha kinakatwa kwa ajili ya kuweza kufanya marekebisho ya matatizo yanayoweza kutokea kwenye mita ya mteja.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilitangaza bei mpya za umeme ambazo zimepanda kwa kuzingatia makundi tofauti. Kulingana na EWURA mwananchi wa kipato cha chini anayetumia uniti (0-75) kwa mwezi, atalazimika kulipia Sh100 kwa uniti ukilinganisha na Sh60 iliyokuwapo awali.
Ongezeko lipo pia katika kundi linaoitwa ‘T1’ la watumiaji wakubwa wa umeme wa nyumbani, ambao watalipia Sh306 kwa uniti ikiwa ni ongezeko la Sh85 ya bei iliyopo sasa. Katika kundi la T2 la wateja wakubwa wanaopimwa kwenye matumizi ya uniti 7,500, malipo ya uniti moja yamefikia Sh205 ikiwa ni ongezeko la Sh73 kutoka bei ya sasa.
Maelekezo ya EWURA yapo wazi inakuwaje TANESCO kuamua kufanya mambo bila kufuata utaratibu kwa kuwa kuna wateja wengi wa TANESCO ambao matumizi ya umeme kwa mwezi mmoja hayazidi unit 75 lakini wamerudishiwa service charge.
Mteja ambaye anatozwa tozo ya huduma uniti moja ya umeme anauziwa kwa gharama kubwa na kupata uniti chache za umeme ambazo hazikidhi kabisa mahitaji ya umeme ya kawaida majumbani kwa ajili ya taa, pasi ya umeme, Jokofu, Kompyuta, Runinga, Redio, kuchaji simu pamoja na matumizi mengine muhimu.
Ukiwauliza TANESCO wanadai wanaoondolewa tozo ya huduma ‘Service charge’ eti ni wateja masikini wasiokuwa na uwezo ambao wananunua umeme wa shilingi zisizozidi 7000 kwa mwezi na kwamba wateja hao masikini ni wale ambao wanatumia zaidi kwa ajili ya taa na sio matumizi mengine.
Kwa maana hiyo iwapo unatumia pasi ya umeme, Jokofu, kuchaji simu, kompyuta pamoja na matumizi mengine muhimu, TANESCO wanakuchukulia kuwa wewe ni mtumiaji mkubwa hivyo wanakuwekea service charge hivyo kulazimika kununua umeme kwa gharama kubwa. Kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu wateja wengi wa TANESCO katika mkoa wa Ruvuma nadhani na mikoa mingine ambao walikuwa wameondolewa huduma ya service charge bila kujali kama anatumia umeme kiasi gani wamerudishiwa huduma hiyo hali ambayo inawaongezea watanzania ugumu wa maisha.
Kitendo hiki kinadhihirisha kuwa Serikali yetu inapenda wananchi wake waendelee kuishi maisha ya kizamani kwa sababu sasa umeme sio huduma muhimu kwa jamii,utapata umeme wa kupimiwa,unatakiwa kutumia taa tu tena ambazo hazitumii umeme mwingi ili usiondolewe tozo ya huduma.