Mlinzi wa Kanisa la ACK All Saints Mountain View lililopo Kangemi nchini Kenya anadaiwa kutoweka na fedha za sadaka kiasi cha Ksh 1.5 ambazo ni takribani shilingi milioni 29 za Kitanzania.
Inadaiwa kuwa, fedha hizo zilikuwa zimechangishwa kama sadaka ili kusaidia maendeleo ya kanisa lakini mipango hiyo ikayeyuka baada ya mlinzi huyo kuvunja sehemu fedha hizo zilikohifadhiwa kisha kutokomea nazo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya, mshukiwa huyo anadaiwa kuiba fedha hizo kutoka kwa madhabahu ya kanisa hilo.
“Wakati mzee wa kanisa John Wainanina na mweka hazina Elizabeth Njoki walipokwenda kanisani kuchukua pesa hizo leo asubuhi, walikuta milango ikiwa wazi, jambo ambalo sio la kawaida."
"Walipotazama kwa makini meza ya Bwana ambapo mkate na divai huwekwa, walishtuka kupata ikiwa imevurugwa na pesa zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye droo chini ya madhabahu hazipo!" DCI alisema.
Wazee hao wa kanisa walipiga ripoti kwa polisi ambao wameanzisha uchunguzi wa kumsaka mshukiwa.
Waumini wa kanisa hilo ambao walighadhabishwa na wizi huo walisikika wakitoa laana kwa mshukiwa huku wengine wakimtaka asamehewe iwapo atajitokeza na kutubu dhambi zake.
