Mwanamke Asha Mwika Gishi aliyekuwa na miaka 35 na mtoto wake wa miezi kumi Precious Paschal wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakiwa kwenye pikipiki maarufu bodaboda walipokuwa wakielekea nyumbani kwao Mishepo.
Marehemu na kichanga chake walipatwa na madhila hayo wakati wakitokea mkoani Morogoro ambapo mama huyo alitoka kufuata vyeti vyake vya kuhitimu Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Ajali hiyo imetokea leo, Jumanne Oktoba 11 jioni katika Mtaa wa Nguzonane, Manispaa ya Shinyanga wakati marehemu akiwa kwenye bodaboda akielekea eneo la magari yaendayo kijijini kwao Mishepo nje kidogo ya Manispaa ya Shinyanga.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzira amethibitisha kupokea mwili wa mama huyo huku mtoto wake akidaiwa kufariki wakati akipatiwa matibabu katika chumba cha uangalizi maalumu.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa, Jackson Mwakagonda amethibitisha uwepo wa ajali hiyo na kusema kuwa dereva wa pikipiki mara baada ya ajali hiyo kutokea yeye alitokomea kusikojulikana huku likimshikilia dereva wa gari lililosababisha ajali.