Chama cha Maendeleo Makete (MDA) jana kimekabidhi serikalini bati 150, mifuko 100 ya saruji pamoja na misumari Ya bati kilo 10 kwa ajili ya ujenzi wa bweni jipya la wavulana shule ya sekondari Mang'oto wilayani Makete mkoani Njombe
Tukio hilo limefanyika shuleni hapo ambapo Makamu mwenyekiti wa chama hicho Philipo Mahenge amesema mbali na Chama cha Maendeleo Makete kuguswa na tukio hilo pia waliwashirikisha wadau mbalimbali ambao nao wamechangia michango yao
Amesema hayo ni miongoni mwa malengo ya MDA kuleta maendeleo kwa wilaya ya Makete kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo, huku akiwapongeza wananchi wa kata ya Mang'oto na Makete kwa ujumla kwa hatua ambazo wamekwisha zichukua tangu tukio la moto lilipotokea shuleni hapo
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa bati hizo Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Veronica Kessy ameshukuru kwa msaada huo na kuendelea kuikumbusha jamii kuwa Maendeleo yataletwa na watu
Mkuu huyo wa wilaya ameshukuru kwa umoja, mshikamano na ushirikiano mzuri uliopo ndani ya chama hicho ambao umewezesha upatikanaji wa vifaa hivyo kwani uamuzi huo wa wanamakete waishio nje ya Makete kupitia MDA umefanikisha jambo hilo
Awali akisoma taarifa ya hatua mbalimbali zilizofikiwa baada ya bweni hilo kuungua Machi 12 mwaka huu, Afisa mtendaji Kata ya Mang'oto Bw. Mengi Chalamila amesema, shilingi milioni sita laki saba sabini na tatu elfu, pamoja na michango mingine ya vifaa kutoka kwa wadau imewezesha ujenzi wa bweni jipya kuanza ambapo ujenzi huo kwa sasa umefikia hatua ya lenta
Nao wanafunzi wanaosoma shuleni hapo wamesema wanashukuru kwa misaada inayoendelea kutolewa baada ya bweni hilo kuungua kwa kuwa yote hayo ni kwa ajili ya wao kusoma katika mazingira mazuri
Baadhi ya wazazi waliozungumza na mwandishi wetu wamesema msaada huo utawasaidia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi huo ambao una umuhimu mkubwa katika elimu
Diwani wa kata ya Mang'oto Mh Osmund Idawa amesema vifaa hivyo walivyokabidhiwa vitafanikisha kuharakisha ujenzi wa bweni hilo
Machi 12 mwaka huu bweni la wavualana katika shule ya sekondari Mang'oto liliteketea kwa moto ambapo ujenzi wa bweni jipya unaendelea na inatarajiwa litakamilika Juni Mwaka huu
Tazama video Hizi:-