Polepole amesema hayo leo Februari 15, 2018 wakati akiongea na waandishi wa habari kuelekea uchaguzi mdogo wa Ubunge na nafasi za udiwani ambao unatarajia kufanyika Februari 17 2018 na kudai kuwa mpaka sasa wamepata taarifa kuwa CHADEMA wanachukua watu kutoka mikoani kuja kulinda kura kitu ambacho hakikubaliki.
"Zipo nyumba kadhaa hapa Dar es Salaam ambazo zimehifadhi watu wasio wakazi wametoka mikoa mbalimbali kuja hapa kwa kigezo cha kulinda kura, sisi hatufanyi siasa za matukio wala kutafuta kiki baada ya kujua hili tumewajulisha jeshi la polisi juu ya nyumba hizo na watu hao, kitakachofuata ni kushugulika na watu hao ambao hawapendi utaratibu mzuri na desturi yetu nzuri ya uchaguzi"
Polepole aliendelea kusema kuwa
"Kura hazilindwi na watu wanaoletwa kwa makundi bali kura kwa mujibu wa Katiba, Sheria ya uchaguzi na kanuni mbalimbali za uchaguzi zimewekewa utaratibu wa kisheria kuhakikisha mwenye yake na anaipata hiyo, upo utaratibu wa mawakala kila chama kina wakala huyo ndiye atakayeshiriki kuhesabu, kujua hii kura yangu au si yangu sasa unapoanza kuandaa watu wasiojulikana na kuwaleta Dar es Salaam ni kuleta taharuki na mpango huo msingi wake ni kutisha wakina mama, vijana na wazee wasijitokeze kwenda kupiga kura, tumesema jeshi la polisi tafadhali tena tafadhali sana watu wasiohusika na usimamizi wa zoezi la uchaguzi ni sheria hawapaswi kuwepo wanatakiwa kuwepo kwenye maeneo yao wakafanye kazi zao za kujiletea kipato, uchaguzi haulindwi na mabaunsa, kura hailindwi bali dola ina vyombo vyake ambavyo sisi wote vyama vya siasa tumekubaliana" alisisitiza Polepole