MWANAMME mmoja mwenye umri wa miaka 20 anazuiliwa katika kituo cha polisi mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta Kenya kwa tuhuma za kumuua mkewe mwenye umri wa miaka 20 baada ya sherehe za krismasi
Jeremiah Mwabiso anashukiwa kuua Bi Miriam Awino baada ya kumdunga kisu mara ishirini na moja.
Akithibitisha kisa hicho , Kamanda wa polisi kaunti hiyo Fred Ochieng amesema kuwa Bw Mwabiso alitenda kisa hicho Jumanne asubuhi katika kijiji cha Ndome -Tausa baada ya sherehe za krismasi.
“Polisi walizuru katika eneo la tukio na kuupata mwili wa mwendazake ukiwa umevuja damu kupindukia..alikuwa na majeraha kadhaa mwilini,” Bw Ochieng alisema.
Bw Ochieng alisema kuwa mwendazake aliuliwa katika kisa ambacho kinasemekana kuwa ni mzozo wa ndoa baina yao .
Kwa sasa mwili wa marehemu unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya rufaa ya Moi mjini Voi huku mshukiwa akisubiri kufikishwa katika mahakama ya Voi leo.
“Repoti za awali zinaonyesha kuwa mwendazake alidungwa kisu mara saba sehemu ya kifua, mara 11 sehemu ya mgongo na mara tatu sehemu ya makalio,” aliongeza Bw Ochieng.
Kufuatia kisa hicho, kamanda huyo ametoa ushauri kwa wanandoa hasa vijana kutafuta ushauri kwa wahubiri au wazee wanapo hitilafiana ili kuzuia visa kama hivi.
Naibu wa chifu wa eneo hilo Chrispus Mwalangi ambaye aliripoti kisa hiki kwa polisi alisema wanandoa hao walitofautiana kabla ya kuanza kupigana,kwani usiku wa kuamkia Jumanne walikesha katika jumba moja la burudani mjini Voi kabla ya tukio hilo.
“Siku ya tukio hilo wawili hao waliondoka kwenye jumba la burudani walipolala wakijiburudisha nakuelekea kwa makaazi yao ambapo mwendazake alianza kuondoa vitu kwa nyumba huku akivichoma,”akaeleza chifu huyo.
Bw Mwalangi alisema wawili hao walioana miezi sita iliyopita na wanaripotiwa kukutana kwa ukumbi wa burudani kabla ya kuamua kuoana.
Kwingineko afisa mwenye mamlaka ya juu anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Port baada ya kukamatwa kufuatia madai ya kujaribu kumuuwa mkewe.
Mkuu wa Kituo (OCS) cha reli SGR upande wa Mombasa James Munuve alikamatwa Jumanne usiku.
Bw Munuve alishikwa baada ya kuripotiwa kufyatua risasi moja kwa jaribio la kumuua mkewe wao eneo la Miritini, Mombasa.
“Afisa huyo anazuiliwa maswali na maafisa wa ujasusi katika kituo cha port. Atapelekwa mahakamani baada ya uchunguzi zaidia,” akasema afisa mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
OCPD wa kituo cha polisi cha port Patrick Lobole alithibitisha kuzuiliwa kwa afisa huyo.
“Yupo kituoni hapa lakini bado sijapata taarifa zaidi kuhusiana na kushikwa kwake. Anaulizwa maswali na maafisa wa ujasusi,” akasema.
Credits: swahili hub