CHIFU wa eneo la Elburgon, Kaunti ya Nakuru Kenya, Jumatano alishambuliwa na kundi la vijana wenye hasira alipoongoza msako dhidi ya pombe haramu.
Bw Francis Ngacha, alikuwa ameandamana na wanachama wa kundi la Nyumba Kumi aliposhambuliwa na vijana hao wakimlaumu kwa kuwaharibia sherehe zao za Krismasi katika Mtaa wa Kasarani, Kaunti Ndogo ya Molo.
“Nilikuwa nimeongoza kikundi hicho kufanya msako dhidi ya maskani za kuuza pombe haramu katika eneo hilo kundi la vijana zaidi ya 10 lilipoanza kuturushia mawe,” akasema Bw Ngacha.
Naibu Kamishna wa Kaunti, Bw Naftaly Korir, alituma kikosi cha polisi wa utawala kufanya msako huo lakini hawakuwakamata vijana waliomshambulia chifu kwani walitoroka.
Polisi walisema wanawatafuta vijana waliohusika ili wachukuliwe hatua za kisheria.