MWANAMKE mmoja anahitaji msaada maalum eneo la Gatundu Kaskazini baada ya nyumba yake kubomolewa na mvua kubwa katika msimu huu wa vuli.
Bi Anne Njeri, 95 alikuwa usingizini mnamo Jumatano alfajiri na wakati alizinduka alipata sehemu moja ya nyumba yake imebomoka.
Bi Njeri ambaye ni mjane amekuwa akiishi peke yake bila msaidizi jambo ambalo limemuacha katika hali ngumu ya kimaisha.
Kulingana na wakazi wa kijiji cha Muiri, Gatundu Kaskazini, eneo hilo limepitia masaibu mengi kwani kila mara huwa kuna mafuriko wakati kunanyesha mvua kubwa.
"Wahandisi wanaokarabati mabomba ya maji katika eneo la Gakoe-Kanyoni wanastahili kufanya juhudi kuona ya kwamba eneo hilo linapata miundo msingi ya kuridhisha. Sisi kama wakazi wa eneo hili tumepitia masaibu mengi sana," alisema Peter Kimani.
Bi Njeri alimpoteza mumewe wiki mbili zilizopita na kwa hivyo si jambo la kuficha kwamba anapitia hali ngumu ya maisha kwa wakati huu.
Mbunge wa eneo hilo Bi Anne Wanjiru Kibe alisema tayari anafuatilia jambo hilo kwa makini kuona ya kwamba wakazi wa eneo hilo wanatengenezewa miundo msingi ya kuwafaidi katika maisha yao ya kila siku.
"Tayari wahandisi wanaorekebisha mabomba ya maji katika eneo hilo wameahidi kumjengea mjane huyo nyumba ya kuishi huku wakiahidi kufuatilia jambo hilo," alisema Bi Kibe.
Kuteseka
Alisema wiki mbili zilizopita kulitokea maporomoko ya ardhi katika eneo la Kanyoni ambapo mimea kadhaa iliharibiwa huku wakazi wakiachwa katika hali ya kutaabika.
Alisema atafanya juhudi azuru baadhi ya maeneo hayo ili kutathmini hasara iliyotokea.
"Wakazi wengi kwa wakati huu wameshindwa kwenda kwa mashamba yao kwa sababu ya 'mvua isiyoisha'," alisema Bi Kibe.
Alitoa wito kwa wananchi kushirikiana ili kuripoti tukio lolote linaloweza kushuhudiwa katika makazi yao.
"Tungetaka wananchi wazungumze kwa sauti moja ili serikali iweze kuwa makini wakati wa kuingilia kati matukio ya aina hiyo," alisema Bi Kibe.
Wakazi wa eneo hilo wameitaka serikali kuingilia kati kuona ya kwamba inawasaidia kurekebisha barabara inayokwenda mashinani, hasa Gakeo na Kanyoni.