Dereva aeleza jinsi Trafiki alivyomvunjia ndoa yake

DEREVA wa kampuni moja ya kushughulikia wageni wanaozuru nchini aliyeshtakiwa kwa kujaribu kumuua afisa wa polisi wa idara ya trafik alidai kortini kwamba afisa huyo alisababisha ndoa yake kuvunjika.
Bw Geoffret Sungura Wekesa alifikishwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani, Nairobi Bw Francis Andayi na kumweleza kwamba yeye (mshtakiwa) ndiye “baba na mama” ya watoto wake kwa vile mke wake alitoroka baada ya kuchumbiana na Konstebo Henry Kemboi.
“Mlalaminishi alinivunjia nyumba. Sasa sina mke. Tumetangana kwa sababu ya vitendo vya afisa huyu wa utumishi kwa wote,” mshtakiwa alimweleza hakimu huku akiomba aachiliwe kwa dhamana “kuwatunza watoto alioachiwa na mke wake.”
Bw Wekesa alikabiliwa na shtaka la kujaribu kumuua Konstebo Kemboi siku mbili zilizopita. Mshtakiwa alidaiwa alijaribu kumuua afisa huyo wa polisi akiendesha gari aina ya Toyota.
Baada ya kusomewa shtaka, mshtakiwa alimweleza hakimu sababu ya kutekeleza uhalifu huo lakini akaambiwa ahifadhi maelezo hayo hadi siku ile atakapoombwa na korti kujitetea.
Konstebo Kemboi ni afisa wa polisi anayehudumu katika kituo cha polisi cha Makongeni kaunti ya Nairobi.
Bw Wekesa alijitetea akisema, “Mheshimiwa hasira ndiyo ilinifanya nitekeleze uhalifu huu. Mlalamishi alibomoa nyumba yangu kwa kufanya urafiki na mke wangu kabla ya kuhamishwa na kupelekwa katika kituo kimoja cha polisi kaunti ya Turkana.”
Matamshi hayo ya Bw Wekesa yalikaririwa na wakili Peter Wakiaga aliyemsihi hakimu amwachilie mshtakiwa kwa dhamana ya kiwango cha juu mno.
“Ni ukweli mshtakiwa alinieleza kwamba mlalamishi alisababisha ndoa yake kuvunjika. Alikuwa akimkonyezea jicho mke wake mshtakiwa na hata kushiriki katika mapenzi haramu,” hakimu alifahamishwa na wakili.
Kiongozi wa mashtaka alimweleza hakimu kwamba, miongoni mwa ushahidi utakaotegemewa ni pamoja na picha za video zilizomuonyesha mshtakiwa akirudisha nyuma gari lake na kuiendesha kwa kasi na kumwangusha mlalamishi.
Kwenye picha hizo mlalamishi anaonekana akianguka juu ya sehemu ya mbele ya gari alililokuwa anaendesha mshtakiwa. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo