Kenya ililalamikia Tanzania kubadilisha sera zake kuhusiana na ujirani mwema, hali iliyoathiri uhusiano kati ya wananchi wa Kenya na Tanzania na biashara kati ya mataifa hayo mawili.
Jumatatu, Katibu Mkuu wa Mahusiano ya Mashauri ya Kigeni Tom Amollo alikosoa hatua ya serikali ya Tanzania kuchoma vifaranga waliokuwa wameagizwa kutoka Kenya na kupiga mnanda ng’ombe waliovuka mpaka wakitafuta malisho.
Bw Amollo alilalamika kuwa Tanzania ilichukua hatua hiyo bila kuhusisha serikali ya Kenya.
Maafisa wa Kenya walilalamikia balozi wa Tanzania nchini Dkt Pindi Hazara Chana, kwa kumwambia hatua kama hizo zilitishia uhusiano wa kihistoria kati ya mataifa hayo mawili.
Kulingana na Bw Amollo, hilo lilikuwa jambo ndogo ambalo lingesuluhishwa kupitia kwa mazungumzo kati ya pande zote mbili.
“Labda kuna haja kubwa ya kuandaa kamati ya pamoja ya wasimamizi maeneo ya mipakani kuzungumzia masuala ibuka,” alisema Bw Amollo wakati wa mkutano huo.
Wiki jana, Tanzania ilichoma vifaranga 6,400 vilivyoagizwa kutoka Kenya kuzuia kuenea homa ya kuku.
Serikali ya Kenya haikufurahishwa na hatua hiyo kutokana na kuwa hakuna visa vya homa ya kuku iliyoripotiwa eneo la mpakani
Chanzo: swahilihub