Mgeni
Rasmi katika utambulisho wa kampeni ya kitaifa kupinga ndoa za
utotoni (National Ending Child Marriage Campaign), Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Anna Maembe, akizungumza na
waandishi wa habari umuhimu wa kufanyia marekebisho sheria ya ndoa ya
mwaka 1971.(Picha na Zainul Mzige).
Na Mwandishi Wetu, MOblog Tanzania
SERIKALI
ya Tanzania imekiri kwamba Sheria ya Ndoa ya 1971 ni kikwazo katika
kupambana na tatizo la ndoa za utotoni na inajipanga kuifanyia
marekebisho ili kulinda haki na sera ya mtoto wa Tanzania iliyopitishwa
na Bunge mwaka 2009.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wakati wa
kutambulisha kampeni mpya ya kitaifa ya kupinga ndoa za utotoni, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Anna Maembe,
amesema kwamba serikali inaridhia kuendesha kampeni ya kupambana na
kuzuia ndoa za utotoni nchini.
“Utafiti
unaonyesha kwamba kati ya wasichana watano wawili kati yao kupata mimba
kabla ya kufikia umri wa miaka 18 kila mwaka nchini Tanzania,” amesema
Bi Maembe
Amesema
kwamba serikali kwa kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa na
wadau wengine wa maendeleo watatizama vyanzo vya ndoa za utotoni kuanzia
kwenye masuala ya kiuchumi, kijamii, mila na desturi na sababu zingine
zinazochangia ukuaji wa tatizo.
“Ndugu
zangu tatizo la ndoa za utotoni si swala la kuachia serikali peke yake
ni kwa kushirikiana na jamii nzima tunaweza kupambana na kuondoa tatizo
la ndoa za utotoni kwa wasichana wa Tanzania,”
Mwakilishi
kutoka, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Idadi ya Watu
Duniani (UNFPA), Dkt. Natalia Kanem akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu utambulisho wa kampeni ya kitaifa ya kupinga ndoa za utotoni
nchini (National Ending Child Marriage Campaign). Kulia ni Mwakilishi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani
(UNHCR), Joyce Mends-Cole na Kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa
Mataifa (UN-Women) nchini, Anna Falk-Collins akifuatiwa na Mgeni Rasmi
katika utambulisho wa kampeni ya kitaifa kupinga ndoa za
utotoni (National Ending Child Marriage Campaign), Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Anna Maembe.
“Na
ukitizama kwa undani wasichana wengi wanapoteza maisha wakati wa
kujifungua ni wenye umri chini ya miaka 18 na wengi wao wanapata
magonjwa ya fistula na ni kundi hatarishi la kupata maradhi ya magonjwa
ya zinaa na ukimwi,” aliongeza
Bi
Maembe aliongeza kwamba serikali inaangalia uwezekano wa kupitia sheria,
sera na mila na desturi katika kuhamasisha jamii juu ya uelewa wa
tatizo la ndoa za utotoni na madhara yake katika ustawi wa jamii na watu
wake.
Alifafanua
kwamba ni muhimu kwa jamii kuanza kubadilika juu ya mila na desturi
zinazochochea ndoa za utotoni nchini ili watoto wa kike wapate nafasi ya
kwenda kusoma hadi vyuo vikuu.
Kwa
upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linalojishughulisha na Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Dkt, Natalia Kanem
amesema kwamba Tanzania ndio ina idadi kubwa ya ndoa za utotoni kwa
wasichana kabla ya umri wa miaka 18.
Alifafanua
kwamba nchini Tanzania mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni mkoa wa
Mara, Shinyanga, Dodoma, Lindi na Tabora kwa hiyo ni muhimu kwa jamii
kuanza mapambano ya dhati dhidi ya mimba za utotoni nchini Tanzania.
“kuna
mambo mengi yanachangia kwa kiasi kikubwa tatizo la ndoa za utotoni
ikiwemo sheria, mila na desturi na sababu zingine za kiimani,”
aliongeza.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TAMWA, Valerie Nsoka (kulia) akizungumza katika hafla ya
uzinduzi wa kampeni maalumu za kitaifa za kupinga ndoa za utotoni
(National Ending Child Marriage Campaign), zitakazoendeshwa Mkoani
Mara.
Amesema
kwamba kupitia kampeni hiyo mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa
kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Wizara
ya wanawake, Taasisi ya Mamna Graca Machel, na Jukwaa la Utu wa Watoto
wataanzisha klabu za mashuleni ili kutoa mafunzo na madhara ya ndoa za
utotoni kwa wasichana nchini nzima.
Dkt.
Kanem amesema kwamba kupitia kampeni hiyo wasichana watafundishwa mambo
ya afya ya uzazi, magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI na madhara ya mimba
za utotoni kiafya na kisaikolojia.
Aliongeza
kwamba tatizo la ndoa za utotoni ni tatizo la dunia nzima kwa mantiki
Umoja wa Mataifa kupitia malengo yake ya millennia iliamua kuweka jambo
la jinsia, afya ya mtoto kama vigezo vya kuondokana na umaskini katika
nchini zinazoendelea.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa TAMWA, Bi Valenrie Msoka amesema kwamba
kampeni hii ni ya kipekee nchini na ni muhimu kwa wadau wote wa
maendeleo kuunga mkono ili kutokomeza kabisa tatizo la ndoa za utotoni
nchini.
Amesema
kwamba kampeni hii itawashirikisha Jeshi la Polisi, Wizara, Viongozi,
Madhehebu ya dini na majaji katika juhudi za kufikisha ujumbe kwenye
ngazi za maamuzi nchini Tanzania.
“Ni
imani yangu kwamba wadau wakubwa katika mapamban dhidi ya ndoa za
utotoni ni waandishi wa habari ambao wana kila sababu ya kuandika na
kuelimisha jamii umuhimu wa mtoto wa kike kupata elimu,” amesema Bi
Msoka.