Wanaokatiwa Bima wanauawa na waliowakatia ili wajitajirishe

IMEFICHUKA kuwa baadhi ya Wakenya wanawaandikisha jamaa zao katika bima za bei ghali na kisha kuwaua ili kupokea mamilioni ya pesa zinazolipwa kama fidia na kampuni za bima.

Ni visa ambavyo vimewashangaza wapelelezi ambao waligundua wakati wakichunguza kundi la walaghai waliovamia sekta hiyo ya bima.

Maafisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Bima (IRA) wa kuchunguza ulaghai pamoja na wapelelezi wa kibinafsi ambao wamekodishwa na wadhamini, waligundua msururu wa visa ambapo watu wanawaandikisha jamaa zao katika bima mbalimbali za maisha pasipo kuwafahamisha, na kisha kupanga njama ya kuwaua ili kulipwa mamilioni ya pesa za fidia kutoka kwa kampuni za bima hizo.
Katika kisa kimoja kilichowaacha wapelelezi vinywa wazi, meneja mmoja wa zamani wa bima alimuandikisha mpwa wake maskini katika bima mbili, lakini inadaiwa kuwa alipanga mauaji ya kijana huyo na kisha mwili kutupwa barabara ya Kangundo kabla kukimbia kudai fidia.
Wachunguzi hao waliozungumza na Taifa Jumapili, walisema mwanamume huyo aliibua tashwishi alipotoa shinikizo chungu nzima kutaka alipwe fidia hiyo akisema alihitaji pesa za kusafiri kuelekea Australia.
Afisa huyo wa zamani wa bima, alikuwa amemchukulia mpwa wake mwenye umri wa miaka 27 bima ya Sh10 milioni na nyingine ya Sh1 milioni katika kampuni mbili tofauti. Alikuwa ametoa mchango mmoja pekee kabla mauaji hayo kutokea.
Mwanamume huyo alikuwa amefanikiwa kukamilisha utaratibu wa kupewa fidia ya bima ya kwanza yenye kitita kinono, na alikuwa katika jitihada za kusaka idhini ya kulipwa fidia ya bima ya pili tashwishi zilipoibuka.
Kumuua mpwa
Ripoti ya wapelelezi ambayo Swahilihub iliona, ilimhusisha mshukiwa huyo katika mauaji ya mpwa wake, ambaye rekodi za simu zilionyesha kuwa wawili hao walikuwa pamoja muda mfupi kabla kijana kutoweka licha ya mshukiwa kukana hayo katika taarifa za kiapo.
Ripoti ya upasuaji maiti iliashiria kijana huyo alifariki kutokana na jeraha mbaya la kichwa lililosababishwa na maumivu yaliyoletwa na kifaa butu.
“Kutokana na uchunguzi, ni bayana kuna ushahidi wa kuashiria kuwepo kwa Mauaji ya Kujitajirisha yanayoendelezwa na wafadhiliwa,” wachunguzi hao walihitimisha katika ripoti yao ya Juni.
Jamaa huyo mshukiwa anasemekana kunaswa na vyeti viwili vya kifo vya nambari mbili tofauti za usajili, ambavyo alinuia kutumia kudai fidia zingine.
Wapelelezi walisema visa hivyo vinazidi kuongezeka huku walaghai wengi wakishirikiana na maafisa wa bima kutayarisha malipo ya fidia bandia, kutokana na mamilioni ya pesa zinazowekezwa katika sekta hiyo ya bima.
Kesi zingine 10 zinazohusu wanandoa, zimeripotiwa na kuibua wasiwasi katika kampuni za bima ambazo sasa zimeamua kuchunguza kiini hasa cha wateja wanaowachukulia jamaa zao bima hususan 'za bei ghali’. 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo