Bw Kung’u mwenye umri wa miaka 40, kutoka kijiji cha Kirima, wadi ya Rurii karibu na Ol Kalou nchini Kenya, alitangazwa mshindi katika shindano hilo la 'Lotto Shinda Mamili Charity”mkesha wa Mwaka Mpya.
Swahilihub ilipomtembelea nyumbani kwake Jumapili, mshindi huyo hakuweza kuficha furaha yake baada ya kujua kuwa alikuwa ameshinda pesa hizo.
“Nilikuwa nyumbani na mke wangu nilipopata kujua kuwa nimeshinda Sh100 milioni. Mwanzoni sikuamini,” alieleza Swahilihub Jumapili asubuhi.
“Niliruka na kuongea kwa sauti ya juu, 'milioni mia moja’, huku nikiwashangaza watoto wangu wadogo ambao hawakuelewa kilichokuwa kikiendelea,” alieleza mwanamume huyo mwenye watoto wawili.
Mara ya kwanza
Alifichua kuwa hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kushiriki mchezo wa aina hiyo na alipata motisha aliposhinda kwanza Sh200 na Sh250 katika mwezi wa Novemba na Desemba.
“Nilianza kushiriki Oktoba na kuendelea kila siku wakati niliweza kumudu gharama yake,” alisema.
Bw Kung’u alisema kuwa atakaa pamoja na familia yake na kujadiliana nayo jinsi ya kuwekeza mamilioni yao.
“Sinaharaka kwa sababu hizi ni pesa nyingi na lazima nipange kwa busara,” alisema.
Aliongeza, Nitakaa na familia yangu na nipate ushauri bora kabla ya kuwekeza. Sote tunajua kuwa sio watu wengi wenye bahati ya kufanya bajeti ya Sh100 milioni. Naomba Mungu anisaidie mimi na familia yangu kutumia pesa hizi vyema.”
Hata hivyo, alisema kuwa sehemu ya pesa hizo ataitumia kuimarisha kilimo chake.
Mchezo huo huwahitaji washiriki kutumia Sh50 kwa kila kiingilia ambapo kiasi cha juu cha kushinda ni Sh100 milioni.
Sportpesa
Mnamo Desemba, mwanamume mwenye umri wa miaka 28 anayefanya kazi ya kuosha magari, alijishindia Sh36 milioni kutoka kwa Sportpesa. Peter Byegon alishinda pesa hizo baada ya kupata matokeo aliyobashiri katika mechi 16 kati ya 17 za ligi ya Uingereza.
Wakati huo aliripotiwa kunusia kwa karibu Sh143milioni iwapo angepata mechi hiyo moja iliyosalia.
Idadi kubwa ya Wakenya wanashiriki michezo hii ya pata potea, ambapo kampuni nyingi zimeibuka na kuuliza maswali hasa kwa upande wa kandanda, huku baadhi ya watu wakitekwa kabisa na michezo hiyo ambayo huwa kushinda ni bahati nasibu.