Uchaguzi wa nafasi ya umeya katika jiji la Tanga umeingia dosari
baada ya madiwani kwa kushirikiana na viongozi wa chama cha wananchi CUF
kupinga matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Tanga
wakidai kuwa yamechakachuliwa hatua ambayo imesababisha askari
kukabiliana na vurugu hizo baada ya msimamizi kukimbia na kwenda
kujifungia ofisini kwake kwa ili kunusuru maisha yake.
Wakizungumza kwa jazba katika uchaguzi huo baadhi ya wafuasi na
viongozi wa chama cha wananchi CUF wamesema hawakubaliani na matokeo
hayo kwa sababu wapiga kura wa CUF walikuwa 20 na wale wa ccm ni 17
lakini katika matokeo hayo msimamizi alitangaza kuwa mgombeanafasi ya
umeya Selemani Mustapher wa CCM amepata kura 19 na Hamad Rashid Jumbe
amepata kura 18.
Wakielezea kwa masikitiko kuhusu mchakato wa uchaguzi huo huku
baadhi yao wakimwaga machozi baadhi ya wakereketwa wa CUF walioshiriki
kuwaapisha madiwani siku moja kabla ya uchaguzi ili wasiweze kurubuniwa
wamesema uchaguzi kama huo unaweza kusababisha maafa kwa sababu haukuwa
wa haki na kweli.
Hata hivyo mgombea nafasi ya umeya kwa tiketi ya CCM Selemani
Mustapher akizungumza katika zoezi hilo amewataka wananchi kuwa watulivu
na ameomba ushirikiano baada ya kutangazwa na msimamizi wa wa uchaguzi
jimbo la tanga Bwana Daud Mayeji.