Ni wakati wa furaha na kusherehekea kwa mwanamke mmoja ambaye hatimaye amejaliwa watoto na kuanza safari ya kuwa mama.
Uwiragiye Marie Chantal aliolewa zaidi ya miaka kumi na nusu iliyopita lakini hakuwahi kujaliwa mtoto. Kwa miaka miwili ya kwanza, alisema majirani na wanafamilia walimhurumia kwa kutozaa. Lakini huku siku zikiendelea kusonga na kuwa miaka mingi ya kungoja bila kupata mtoto, alianza kudharauliwa na kudunishwa.
Akisimulia Afrimax English hadithi yake, Uwiragiye alisema alisemwa vibaya kwa kutomzalia mumewe mtoto.
"Walisema sikuwa na nyumba ya mtoto. Ilikuwa safari yenye changamoto kwani wakati fulani mume wangu alitaka kuniacha hadi muujiza utokee maishani mwangu," mama huyo wa watoto wanne alisema. Alifurahi kuwa mume wake alikubali kusimama naye kama alivyoahidi hado walipojaliwa watoto wanne wa kupendeza baada ya miaka 15 ya kujaribu na kusubiri. Marie alifichua kwamba alikuwa amekata tamaa ya kuwa mama kwani awali alipoteza mimba tano. Hata hivyo, mnamo Disemba 25, 2022, alipokea zawadi nzuri zaidi ya Krismasi ambayo mwanamke akiwazaa Phares, Otis, Amora, na Anaya. "Nilizidiwa sana hata sikuweza kuiwaza kabisa, niliogopa sana mimba hii isifanikiwe. Hata mimi nilikubali tu kuwa nina watoto baada ya kujifungua." "Ilikuwa ni wakati wa furaha sana. Nilishangaa sana. Ilikuwa ni muujiza. Sikuamini," alisema.
Chanzo: TUKO.co.ke