MKAZI wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, John Albin, amenusurika kufa kwa kushambuliwa na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, baada ya kusadikiwa kuwa ni mwizi wa pikipiki.
Kaka wa majeruhi huyo, Godwin Albin, ambaye anamuuguza katika Hospitali ya Huruma iliyopo Rombo, amesema tukio la kushambuliwa kwa mdogo wake lilitokea saa tano mchana, katika eneo la Kiboro wilayani humo na kumsababishia majeraha makubwa kichwani.
Albin anasema, wakati tukio hilo linatokea, mdogo wake alikuwa akitoka Tarakea akiwa anaendesha pikipiki ambayo ni mali yake yenye namba za usajili MC 283 BEN aina ya Boxer.
Baada ya kufika eneo la Kiboro madereva wanaopaki eneo hilo walimtilia shaka kuwa ni mwizi, kisha kuanza kumshambulia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbroad Mutafungwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Amesema, wakati tukio hilo likiiendelea polisi walifika eneo la tukio na kumuokoa majeruhi huyo pamoja na fedha alizokuwanazo zaidi ya Sh milioni 3.3.
Mutafungwa amesema, kwa kuwa majeruhiwa kuwa katika hali mbaya, Polisi walimkimbiza katika hosptali ya Huruma kwa ajili ya matibabu.
Baada ya muda watu wawili, Proches Mrema mwenye umri wa miaka (18) na Victor Edward mwenye umri wa miaka (30) walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
Mutafungwa amesema, Polisi inalaani kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi, na amewataka wananchi wa eneo hilo kutoa taarifa za watu wengine waliohusika na tukio hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mganga Mkuu wa Hosptali ya Huruma, Wilbroad Kyejo, amethibitisha kumpokea majeruhi huyo akiwa katika hali mbaya.
Anasema, alikuwa ameumia zaidi maeneo ya kichwani, na kwamba, jitihada za kumuhamishia katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC zinaendelea kwa ajili ya kupata vipimo zaidi hususani maeneo ya kichwa.
HABARI LEO