Mbunge aeleza jinsi Maji yanavyovunja ndoa za watu Huko Chunya

MBUNGE wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), ameitaka serikali kueleza ni lini itapeleka maji ya uhakika katika miji ya Makongorosi na Chunya kwa kuwa ndoa za wakazi wa maeneo hayo ziko hatarini kuvunjika kutokana na wanawake kufuata maji umbali mrefu na kutumia muda mwingi.
Mwambalaswa amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji kuongozana naye mpaka katika maeneo hayo baada ya Mkutano wa Bunge ili kujionea matatizo wanayopata wanawake kusaka maji ya visima kuanzia saa 10 alfajiri na muda wanaotumia.
Aliyasema hayo bungeni jana alipouliza wizara hiyo swali la nyongeza kuwa ina nia gani kunusuru ndoa za watu katika eneo lake zinazotaka kuvunjika kutokana na tatizo la maji.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isaack Kamwele amesema serikali inatambua tatizo la maji katika mji wa Makongoroso na Chunya na kwamba kuna eneo serikali inaliangalia ili kuona kiasi cha maji kilichopo kama kinaweza kusambazwa maji maeneo hayo.
Katika swali la msingi, Mwambalasa aliuliza, “Katika mpango wa Serikali wa kuchimba visima vya maji katika vijiji 10 vya kila Halmashauri, katika mji mdogo wa Makongorosi maji hayakupatikana kwenye kisima”.
Alihoji serikali itachukua hatua gani kutatua tatizo hilo hasa kutokana na mji huo kukuwa kwa kasi na kero ya maji ni kubwa.
Naibu Waziri Kamwele akijibu swali hilo, alisema mradi wa maji katika mji mdogo wa Makongorosi ni moja ya miradi ya awali iliyopewa kipaumbele kutekelezwa kwenye mpango wa vijiji 10 kwa kila halmashauri.
“Baada ya maji kukosekana kwenye kisima kilichochimbwa, mradi huu haukuweza kuendelea kutekelezwa na jitihada za kutafuta chanzo kingine zinaendelea,” amesema.
Amesema mradi wa maji wa Makongorosi, umepangwa kutekelezwa upya katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambapo kwa mwaka 2016/17, Halmashauri ya Chunya imepangiwa bajeti ya Sh milioni 561.5.
Alisema kazi zilizopangwa kufanyika ni kutafuta chanzo kingine kufanya usanifu na ujenzi wa miundombinu ya mradi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo