Tanzania imekuwa mshirika mkubwa wa Marekani kwa miaka mingi na katika siku za karibuni, Tanzania imenufaika na misaada ya mabilioni ya shilingi katika sekta za elimu, afya, maji, miundombinu ya barabara na nishati ya umeme.
Bungeni Dodoma, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amempongeza mgombea huyo wa chama cha Republican, Trump kwa kushinda nafasi hiyo na kuwa rais mpya wa Marekani.
Aidha, Dk Ackson amesema yeye binafsi na wabunge wengine wanawake, wamesikitishwa na kushindwa kwa mgombea urais wa Democrat, Hillary Clinton.
Naibu Spika aliyasema hayo jana bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu, wakati akitambulisha wageni. Alisema walitarajia kwamba mambo yangekuwa mazuri kwa upande wao (wanawake), lakini haikuwezekana.
“Nachukua nafasi hii kumpongeza Trump kushinda uchaguzi wa Marekani, Hillary hakuweza labda baada ya miaka minne ijayo. Tunatambua juhudi zake na amejitahidi sana,” alisema Dk Tulia huku akishangiliwa na wabunge wengi wakiwa wanawake. Akifanya utani, Dk Tulia alisema, “Nasikia kuna watu hapa wanasema tungempeleka mheshimiwa fulani… katika maeneo yale mama Clinton angeshinda,” alisema na kushangaliwa.
Awali, wakati wa kipindi cha maswali jana, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema) alisema ana masikitiko makubwa kwa sababu Hillary ameshindwa.
“Kwa niaba ya wanawake wenzangu nampa pole Mama Clinton. Tumeumia na tumerudi nyuma,” alisema Lyimo na Naibu Spika alimuuliza amepata wapi hiyo taarifa wakati walikuwa na matumaini Hillary angeshinda.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla akijibu swali la Lyimo, alimpa pole Hillary kwa kushindwa katika uchaguzi huo.
Alisema yeye ni Balozi wa Wanawake, anawapenda wanawake na kwa sababu hiyo anampa pole mgombea huyo wa Democrat kwa kushindwa na anampongeza Trump kwa ushindi. Wamarekani walipiga kura juzi kumchagua raia atakayemrithi rais wa sasa, Barack Obama.