Viongozi wa mila kutoka jamii ya kifugaji katika kijiji cha Naberera wilaya ya Simanjiro wameanza kutekeleza adhabu ya kuchapa bakora sabini kwa wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao ili kukomesha tabia hiyo inayochangia kuongezeka kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwenye kijiji hicho.
Wakizungumza na vijana wa jamii ya kifugaji wazee na viongozi wa mila wamesema wamefika hatua hiyo baada ya kuongezeka kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji inayotokana na tabia ya baadhi ya wafugaji kutofuata taratibu.
Baadhi ya watendaji wa serikali kata ya Naberera wamesema tabia hiyo imeleta madhara kwa jamii hizo mbili lakini tayari wameunda kamati ya kuondoa migogoro hiyo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Naberera Jacob Korosi ametumia nafasi hiyo kuwaonya wafugaji kuacha tabia hiyo kwakuwa watanzania wana haki sawa kwenye ardhi bila kujali anatoka jamii gani.
