Hatimaye miili ya waliokua watafiti katika kituo cha utafiti wa kilimo Seliani waliochomwa moto hadi kupoteza maisha wilayani Chamwino mkoani Dodoma wakati wakiwa katika utafiti wa udongo imewasili mkoani Arusha huku watafiti wenzao wakiitaka serikali kuchukua hatua kali za kisheria kwa waliotekeleza mauaji hayo.
Mnamo majira ya saa mbili asubuhi ya oktoba tatu miili hiyo imewasili katika makao makuu ya kituo hicho na kupokelewa na watumishi wenzao pamoja na ndugu na jamaa wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya maafa hayo Bwana Philemon Mushi.
Baadaye miili hiyo ikapelekwa kuhifadhiwa kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti ya hospitali ya Mount Meru kusubiri taratibu za mazishi ambapo mwili wa aliyekua dereva Nicas Magazini unatarajiwa kusafirishwa kwenda Ifakara Morogoro na kijana Faraji Mafuru ukisafirishwa kuelekea wilayani Bunda mkoani Mara huku mwili wa marehemu Theresia Ngoma ukitarajiwa kuzikwa jijini Arusha.
Daktari Januari Mafuru ndiye mkurugenzi wa kituo hicho cha utafiti cha Selian ambaye pia amempoteza mtoto wake Faraja Mafuru anasema ipo haja kwa jamii kuelimishwa na kutambua kuwa utafiti wa udongo unaofanywa na watafiti ni kwa maslahi ya jamii na taifa zima katika kuinua kilimo.
Tukio la kuuawa na kuchomwa moto kwa watafiti hao linaelezwa kutokea siku ya jumamosi Oktoba mosi majira ya mchana katika kijiji cha Iringa wilayani Chamwino kwa kile kinachodaiwa kutekelezwa na wananchi baada ya kuamini kuwa watafiti hao waliokua kwenye utekelezaji wa majukumu yao walikua ni wanyonya damu.