Vitendo vya unywaji pombe kupita kiasi vimeendelea kuleta
madhara wilayani Makete mkoani Njombe baada ya kijana Edward Sanga (20)
kufariki dunia kutokana na kunywa pombe kupita kiasi
Kwa mujibu wa taarifa za mashuhuda zinasema kuwa tukio
hilo la unywaji pombe kupita kiasi limetokea jana Usiku katika kijiji cha
Lupalilo Wilayani hapa baada ya kijana huyo aliyekuwa na rafiki yake kunywa
pakiti 14 za pombe aina ya Valuu na kuondoka kilabuni hapo ndipo leo asubuhi
kukutwa maeneo ya kilabuni hapo akiwa Amefariki dunia
Bi Bertha Henigen Ni Afisa mtendaji wa kata ya Lupalilo
anazungumzia namna tukio hilo lilivyotokea Kwa kusema kiwango kikubwa cha pombe
alichokunywa ndicho kimepelekea kifo cha kijana huyo
Muhudumu wa kilabu alipokuwa akinywa pombe marehemu kabla
umauti kumfika Bi Juliana Sanga amesema ni kweli alikuwa akinywa pombe kilabuni
hapo na baadaye kuungana na rafiki yake ambaye alimnunulia pombe hizo
Mmiliki wa Kilabu cha pombe alipokuwa akinywa pombe
marehemu kabla ya kupoteza maisha Bw. Chesko Sanga amezungumzia tukio hilo
pamoja na diwani wa kata hiyo Mh Imani Mahenge ambaye amesema kata yake
imempoteza kijana aliyekuwa tegemeo katika shughuli za maendeleo kijijini hapo
huku pia akitoa onyo kwa vijana wenye tabia kama hiyo kuacha kupoteza muda wao
kunywa pombe kupita kiasi na badala yake wajikite kujenga nchi kupitika
shughuli mbalimbali zilizohalalishwa na sheria za nchi
Baba Mdogo wa marehemu akizungumza na mwandishi wetu
amesema wamekuwa wakimuonya kijana wao kuhusu unywaji wa pombe kali ambazo
alikuwa akinywa kwa kujificha bila wao kujua ingawa jitihada zao kama familia
hazikuzaa matunda
Jeshi la polisi lilifika eneo la tukio na kuukagua mwili
wa marehemu ambao haukukutwa na jeraha lolote na kugundulika kuwa kifo cha
marehemu kimetokana na kunywa pombe kali maarufu kama viroba kupita kiasi, na
kuruhusu familia kwenda kuzika mwili huo, huku wakisisitiza Wamiliki kuzingatia
muda wa kufunga vilabu vya pombe uliowekwa kisheria
