Inadaiwa askari huyo aliyechomwa
kisu shingoni Jumapili katika kijiji cha Matare, kauntindogo ya Kuria
Mashariki, alishindwa kulipa deni hilo.
“Tumewahoji walioshuhudia mkasa huo
na kubainisha kuwa chanzo ni deni hilo wala sio mgogoro wa kimapenzi
kama ilivyoaminika hapo awali,” alithibitisha Mkuu wa Polisi katika
Kaunti ya Migori, David Kirui.
Duru zinaarifu kuwa deni hilo lilitokana na chang’aa aliyokunywa afisa huyo.
Mshukiwa wa mauaji hayo ambaye ni
mpenzi wa mjane anayeuza chang’aa hiyo, alichomoa kisu kutoka kwenye
koti lake na kumshambulia askari huyo ambaye alifariki dunia kabla ya
hata kuwasili hospitalini.
Mshukiwa pamoja na mjane huyo walitoroka punde tu baada ya tukio hilo. Inasemekana wametokomea nchi jirani ya Tanzania.
“Tumeanza kuwasaka kwenye maeneo ya mpaka wa Kenya na Tanzania,” alisema Bw Kirui.
Maiti ya mwathiriwa ilipelekwa katika hospitali ya rufaa ya Migori itakapofanyiwa uchunguzi zaidi.
Kwingineko, mwanamume mwingine
alifariki dunia baada ya kudungwa kisu na mpenzi wake mjini Maragua,
Kaunti ya Murang’a baada ya kuzuka mtafaruku baina yao.
Mwili wa Peter Njoroge, 38
ulipatikana umelazwa kwenye kidimbwi cha damu Jumapili iliyopita huku
majeraha ya kisu yakienea kwenye upande wa kushoto wa kifua chake.
Mshukiwa, mama wa watoto watatu, alitiwa mbaroni na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Murang’a huku uchunguzi ukiendelea.
“Uchunguzi unaashiria jamaa huyo
alikuwa akimdai Sh19,000 kabla ya mwanamke huyo kuchomoa kisu na
kumchoma mara kadhaa,” alisema chifu wa eneo hilo Ali Mzee.
Bw Ali alisema wawili hao waliishi pamoja kwa miezi kadhaa lakini hakuthibitisha kama waliwahi kuoana.
Hata hivyo, alisema kuwa wamekuwa wakizozana mara kwa mara.
“Tunachofahamu ni kuwa mwanamke
huyo alimzidi umri marehemu na alikuwa na watoto watatu hata kabla ya
kuanza uhusiano wake na Njoroge,” alisema chifu huyo.