Kijana ajichimbia kaburi ajizike baada ya kukosana na babake

MVULANA aliyechimba kaburi lake na kusema alikuwa tayari kufa baada ya ugomvi wa kinyumbani na babake, alitiwa mbaroni Jumamosi na maafisa wa usalama kwenye kaunti ya Kakamega.
Kisa hicho kimewaacha wanakijiji kutoka kata ya Shirumba, eneobunge la Ikolomani wakiwa na mshangao na hofu. 

Mshukiwa Nelson Ambia Malaya, 19 alitoweka nyumbani kwao Jumatano iliyopita baada ya kuzua taharuki kwa kufukua kaburi la shangaziye marehemu na baadaye kuchimba kaburi lake huku akitishia kujitoa uhai.


Baadaye, aliwashambulia na kuwakata fahali watatu wa babake na kufweka mimea ya mahindi na miwa kwenye shamba la jirani huku akitoa vitisho kuwa angelimua dadake wa umri wa miaka 13, ambaye ni mwanafunzi katika shule ya msingi ya Malinya.
Mshukiwa anazuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Malaika, eneo bunge la Ikolomani akingoja kufikishwa mahakamani jumatatu.

Babake mshukiwa Henry Malaya, aliambia Taifa Jumapili kuwa amekata tamaa baada ya mwanawe kujihusisha na vitendo vya uhuni. Alisema mwanawe alikuwa na pupa ya kutaka vitu vya bure bila ya kutoa jasho.

“Ningependa hatua kali ichukuliwe dhidi ya mshukiwa kwani ametishia kuwa atatuua na kuchoma nyumba zetu. Sielewi kwa nini ameamua kujihusisha na uhalifu,” alisema Mzee Malaya.

Mshukiwa alikuwa anatumikia kifungo cha nje baada ya kuwatishsia maisha wazazi wake mwaka jana na kuchoma nyumba mbili kwenye boma la babake.

Chifu wa kata ya Shirumba Bw Eustace Butichi, alisema kuwa mshukiwa alikuwa ameenda mafichoni baada ya kukosa kujiwasilisha kwa afisi yake kama alivyo agizwa na mahakama.
“Mahakama ilitoa kibali cha kumkamata baada yeye kutoweka na kukosa kutoa huduma inayo ambatana na kifungo cha nje ya jela,” alisema Bw Butichi.
Mzee Malaya alisema hakuna tambiko jamii yake inapanga kufanya ili kuondoa kisirani nyumbani kwake, kwani mwanawe hajaonyesha kujuta kwa kitendo alichofanya.
“Sioni haja yoyote ya kufanya tambiko ili kusafisha mji wangu kwani mwanangu hajuti kwa yote aliyo fanya. Naomba mahakama imuchulie hatua kali,” alisema Bw Malaya.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo