VIGOGO
wawili wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) wanaokabiliwa na mashitaka ya
kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 1.2 wameachiwa kwa dhamana.
Washitakiwa
hao ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara, Avelin Momburi na Mkurugenzi
wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph
Makani.
Hata
hivyo, washitakiwa wengine akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Mamlaka hiyo, Dickson Maimu na wenzake watano wanaendelea kusota
rumande.
Hakimu
Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Respicius Mwijage alitoa
uamuzi huo jana kwa kuwa washitakiwa hao wawili hawaguswi katika
mashitaka yaliyofunguliwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Alisema
anakubaliana na hoja za upande wa utetezi zilizowasilishwa na Wakili
Johnson Jamhuri kuwa mashitaka yanayowakabili washitakiwa hao yana
dhamana na hayahitaji kuombewa dhamana hiyo Mahakama Kuu.
Hakimu
Mwijage alisema, washitakiwa wanatakiwa kila mmoja kuwa na wadhamini
wawili ambao watasaini hati ya Sh mil 200, pia wawasilishe hati zao za
kusafiria na hawatakiwi kwenda nje ya Dar es Salaam bila kibali cha
mahakama.