Mkuu wa polisi aeleza mahakamani Mwalimu alivyomtukana

Mkuu wa Polisi Wilaya Misungwi (OCD), Slvester Ibrahim ameieleza mahakama jinsi Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbela, Salome Lufungulo (35) alivyomtukana kuwa mpumbavu.

Ibrahim alikuwa akitoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza ambayo imeanza kusikiliza kesi inayomkabili Lufungulo ya kutoa lugha ya matusi kwa simu kwa mkuu huyo wa polisi.

Ibrahim ambaye ni shahidi wa kwanza upande wa mashtaka akiongozwa na mwendesha mashtaka wa polisi, Doroth Mgenyi alidai kuwa Oktoba 5, mwaka jana saa mbili usiku akiwa ofisini alipokea malalamiko kutoka kwa Sajenti Yuston yaliyomshinda kuyapatia suluhu.

Alidai malalamiko hayo yalikuwa ya Mama Kimario dhidi ya Mwalimu Lufungulo kumtolea lugha ya matusi huku akimtuhumu kutembea na mumewe.

Shahidi huyo alidai alimpigia simu Lufungulo huku akijitambulisha kuwa ni OCD, lakini mwalimu huyo alianza kumtukana na kumkashifu.

Alidai walimrekodi mwalimu huyo kwa kutumia simu ya mkononi ya ofisa upelelezi makosa ya jinai Wilaya ya Misungwi, Wilson Kisura.

“Hata ukinirekodi OCD, unakiherehere, wewe ni mpumbavu, umekula rushwa ya ngono, huko siji najua mtanipiga mabomu, ndiyo maana vituo vya polisi vinachomwa moto kwa ajili hiyo, nitakufukuzisha kazi,” alidai shahidi huyo wakati akinukuu maneno ya mtuhumiwa.

Hakimu mkazi mfawidhi, Ruth Mkisi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 10 itakapoendelea kusikilizwa kwa upande wa mashtaka kutoa ushahidi. 

Mshtakiwa huyo yuko nje kwa dhamana.

chanzo: mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo