Askofu Aliyefunga Siku 40 Afia Chumbani

 Mwili wa maehemu Askofu wa Kanisa la Taliteha, Ubungo jijini Dar, Fred Mwarusi ukiwa kwenye gari la polisi.

Waandishi wetu, Amani
DAR ES SALAAM: Imefichuka!  Kifo cha Askofu wa Kanisa la Taliteha, Ubungo jijini Dar, Fred Mwarusi (45) kilichotokea chumbani kwake, Makuburi, Jumapili iliyopita kimezua mengi na mazito, Amani limefuatilia kwa kina.
 Mwili wa marehemu huyo ulibainika na majirani baada ya kusikia harufu kali kutokea kwenye chumba chake kutokana na kutomwona akiingia wala kutoka kwa siku kadhaa.
Mwili wa marehemu ukiagwa.

 Kwa mujibu wa chanzo makini, kabla ya kifo chake, Askofu Mwalusi alijifungia chumbani mwake kwa siku kadhaa nyuma kwa ajili ya kufanya maombi ya uponyaji kwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua ambayo hayajajulikana mara moja.
 ALIKATAA KWENDA HOSPITALI

“Askofu Mwalusi alikuwa akisumbuliwa na maradhi f’lani hivi, yalimfanya afya yake kudhoofu. Majirani zake na  waumini wake walimshauri mara kwa mara kwenda kutibiwa hospitali ili arejeshe afya yake, lakini alikuwa akigoma kwa maelezo kwamba, atafanya maombi, atapona kwa Jina la Yesu.
 “Alikuwa akisema dawa pekee kwenye matatizo yake ya kiafya ni maombi tu na kuonesha kuwashangaa sana waliokuwa wakimshauri habari ya kwenda hospitali,” kilisema chanzo.
 Kanisa la Taliteha

MMOJA WA MAJIRANI ANENA
Akizungumza na Amani juzi kwenye msiba wa askofu huyo, mmoja wa majirani zake aliyekataa katakata jina lake kuandikwa gazetini, alisema siku ya mwisho kumuona marehemu huyo ilikuwa Ijumaa ya Julai 29, mwaka huu ambapo aliingia ndani kwake halafu akasikika akifanya maombi kwa kumuomba Mungu ampe afya njema.
 “Nilimsikia akimwomba Mungu ampe afya njema. Lakini baada ya maombi hayo ya nguvu, nikamsikia akikemea pepo kwa sauti ya chini sana kisha sikumsikia tena mpaka leo (Jumapili) ndiyo tukaanza kusikia harufu ikitoka chumbani.”
 WASIWASI ULIANZA
“Lakini kuna wakati tuliingiwa na wasiwasi kwa kutomuona mwenzetu akifungua mlango wake tangu Ijumaa jambo ambalo halikuwa la kawaida kwake. Alikuwa mtumishi wa Mungu mwenye harakati za kiroho kila wakati, akiingia na kutoka, pengine akiwa anaimba nyimbo mbalimbali.”
 “Kufuatia hali hiyo, tuliambizana kuwa tupige simu polisi ambao walifika hapa na kuvunja chumba chake, wakamkuta amefariki dunia,” alisema jirani huyo.
 SERIKALI YA MTAA
Akizungumzia tukio hilo Jumatatu iliyopita, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makuburi Kibangu, Moshi Kaftani alisema alipewa taarifa za kifo cha mtumishi huyo wa Mungu na mmiliki wa nyumba, Peter Mrema ambapo alishirikiana na polisi kuvunja mlango na kumkuta ameshafariki dunia huku kukiwa na harufu kali chumbani humo.

“Huyu marehemu ni mwananchi wangu ambaye alikuwa askofu na baadhi ya waumini wake ni wale pale unaowaona na wachungaji wake walikuwepo hapa lakini sasa hivi wameshaondoka.”

 ALIKATAA KUOA MPAKA…
“Marehemu licha ya kuwa na umri wa miaka 45 lakini hakuwa na mke wala mtoto. Alipokuwa akiulizwa sababu ya kuishi bila mke alisema anasubiri aoteshwe na  Mungu kwa kuoneshwa ndotoni ndiyo amuoe.

“Licha ya kuisubiri ndoto hiyo kwa muda mrefu lakini haikuwa imemtokea mpaka umauti ulipomfika,” alisema mwenyekiti huyo.

 POLISI WATOA MWILI, MAJIRANI WALIA
Paparazi wetu aliushuhudia mwili wa baba askofu ukitolewa nyumbani hapo alipokuwa akiishi na Askari wa Kituo cha Polisi Mbezi Louis jijini Dar kwa ajili ya kwenda kuufanyia uchunguzi huku majirani zake wakisikitika, wengine wakilia kwa uchungu.
MZOZO WA MAZISHI?
Juzi Jumanne, kulidaiwa kuibuka kwa mzozo wa eneo sahihi la kumzikia marehemu huyo ambapo, baadhi ya ndugu walisema asafirishwe kwenda Mbeya lakini mama wa marehemu akisema azikwe jijini Dar. Hata hivyo, mwenyekiti wa serikali ya mtaa alikanusha kuwepo kwa mzozo.

Mwili wa marehemu ulizikwa Jumanne iliyopita kwenye Makaburi ya Ubungo Maji jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na waumini wake, majirani na wachungaji huku ibada ya mazishi ikiongozwa na Askofu David Mwasota wa Kanisa la Naioth Gospel Assembly la jijini Dar.


KAMANDA WA POLISI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo bila kufafanua zaidi.

Waandishi: Richard Bukos na Gladness Mallya.


Source: Global Publisher


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo