ASKARI jela aliyempiga risasi na kumjeruhi vibaya msichana wa
shule ya upili Kaunti ya Migori, Ijumaa iliyopita, sasa amesimamishwa
kazi.
Mkuu wa polisi wa Kaunti hiyo, Bw David Kirui, alisema afisa huyo alisimamishwa kazi baada ya maafisa kutoka makao makuu ya idara ya magereza jijini Nairobi kufika jela la Migori kufanya uchunguzi.
“Alipokea barua ya kumsimamisha kazi na hayuko kazini sasa,” Bw Kirui aliambia SwahiliHub Jumapili. “Atafikishwa kortini baada ya uchunguzi kukamilika na tayari ameandikisha taarifa kuhusu kisa hicho cha ufyatulianaji risasi kilichotokea wiki jana,” afisa huyo aliongeza.
Bw Kirui alisema hayo wakati ambapo mkuu wa upelelezi wa Kaunti hiyo Bw Benedict Kigen, alikuwa njiani kwenda hospitali ya rufaa ya Eldoret msichana huyo mwanafunzi wa kidato cha pili anakotibiwa.
“Ataenda kuandikisha taarifa kutoka kwa mwanafunzi huyo wa shule ya wasichana ya Ulanda kama sehemu ya uchunguzi,” aliongeza Bw Kirui.
Aliwataka maafisa wa usalama kuwa makini wanapotumia silaha kwa sababu watachukuliwa hatua kali za kisheria wakizitumia vibaya.
Askari jela huyo alikuwa akimfuata mfungwa aliyetoroka mjini Migori Ijumaa iliyopita alipompiga risasi na kumjeruhi msichana huyo, tukio ambalo lilifanya wakazi kuandamana.
Msichana huyo alipigwa risasi jichoni akitazama mashindano ya mpira katika shule ya wavulana ya Migori. Mfungwa huyo aliingia katika uwanja wa shule hiyo huku askari jela huyo aliyekuwa na wenzake wakimfuata.
