Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitilla Mkumbo amesema
kuna mambo mawili yanayoibana Serikali katika mgogoro wa wanafunzi
waliotimuliwa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Akizungumza
jana kwenye kipindi cha ‘Kipima Joto’ kinachorushwa na kituo cha
luninga cha ITV, Profesa Mkumbo alisema Serikali haiwezi kukwepa lawama,
kwa sababu ndiyo iliyoanzisha utaratibu wa kudahili wanafunzi wa kidato
cha nne kupitia mfumo maalumu kabla ya kuanza kusoma shahada ya chuo
kikuu.
Pia,
alisema Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), haiwezi kuhusika moja kwa
moja kwenye udhaifu uliojitokeza katika udahili wa wanafunzi hao, bali
Seneti ya Udom inapaswa kuwajibika katika hilo.
Alisema
kuna udhaifu wa kiutendaji kwa seneti hiyo yenye mamlaka ya kudahili
wanafunzi wenye sifa ambayo iliiacha kazi hiyo mikononi mwa TCU.
Mkumbo alisema kazi ya TCU ni kuidhinisha majina ya wanafunzi waliokwisha dahiliwa na chuo husika na si kuchagua.
“Chuo
chochote ndicho kinachagua wanafunzi wenye sifa wanazozihitaji,
inashangaza kuona Udom imefanyiwa kazi hiyo, baraza na seneti wanapaswa
kuwajibika kwanza, TCU haiwezi kukichagulia chuo wanafunzi,” alisema Profesa Mkumbo.
Hata
hivyo, alitoa angalizo kwa Serikali kutodharau mfumo huo wa udahili kwa
wanafunzi ambao hawakuhitimu Kidato cha Sita kama ilivyoamriwa na
Serikali ya Awamu ya Nne, kuwa upo na unatumika duniani kote.
“Ila
kama Rais (John) Magufuli hautaki na ameona turudi kwenye mfumo wa
zamani ambao mwanafunzi anapaswa kufaulu kidato cha sita ndiyo ajiunge
na chuo kikuu sawa, lakini atambue kuwa kuna hasara na faida zake, vyuo
vingi vinaweza kufungwa,” alisema Mkumbo
Mbali
ya mfumo huo, profesa huyo alisema upo mfumo mwingine wa udahili kwa
mtu yeyote mwenye umahili katika taaluma yake kusoma shahada kwa
kuzingatia vigezo maalumu vilivyowekwa.
“Ila hakuna jinsi, nadhani TCU wamemsikia Rais kuwa hataki njia za mkato tena.”
Mei
29, Udom iliwasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu
ya ualimu wa sayansi kwa ngazi ya stashahada na kuwataka waondoke
chuoni mara moja.
Amri
hiyo iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, ilisema Serikali imeamua warejee kwao na wataelezwa mustakabali
wao mapema iwezekanavyo.
Hata
hivyo, Rais John Magufuli juzi alisema baadhi yao walikuwa vilaza,
hivyo wajitafutie mahali pa kwenda huku wenye ufaulu wa daraja la kwanza
na pili aliahaidi kuwa wataandaliwa utaratibu.