WABUNGE
watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Dk Abdallah Possi
ambaye ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,Kazi,
Ajira, Vijana na Walemavu), wameutaka umma uelewe kuwa shinikizo la
wapinzani bungeni kuhusu utendaji wa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson lina
uonevu wa kijinsia.
Katika
mkutano huo na wanahabari uliofanyika ofisi za Waandishi wa Habari,
bungeni mjini Dodoma jana, Dk Possi aliongozana na Mbunge wa Muleba
Kusini, Profesa Anna Tibaijuka na Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, walisema hawakubaliani na mkakati wa kambi ya
upinzani kutaka kumng’oa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, kwa sababu ni
mkakati wenye shinikizo la kisiasa na ubaguzi dhidi ya wanawake.
Dk
Possi alisema wabunge wa kambi ya upinzani hawana hoja za msingi kutaka
kutekeleza mkakati wao huo kwa sababu si mara ya kwanza kwa wanaokiuka
kanuni na taratibu za Bunge kutolewa au kusimamishwa.
“Tunaamini
kinachotokea sasa ni msukumo wa kisiasa kwa kuwa wabunge wana njia ya
kufanya kuwasilisha malalamiko yao, ikiwa wanaona wameonewa na si
kupanga mkakati wa kumtoa madarakani wanayeamini anawakosea. Wana nafasi
ya kukata rufaa,” alisema Dk Possi.
Profesa
Tibaijuka alisema wakati Samwel Sitta akiwa Spika aliwatoa wabunge
wasiofuata kanuni na hakukuwa na yanayotokea sasa, jambo linaloonesha
kuwa wanamlenga Dk Tulia kwa sababu ni mwanamke.
Kakunda alisema anaamini pia kuwa maamuzi hayo ya kambi ya upinzani yana msukumo wa kisiasa kwa sababu hoja zao hazina msingi.