Wakati zoezi la upimaji ardhi likiendelea katika kata ya Tandala Wilayani Makete wananchi wamekumbushwa juu ya haki ya umiliki wa ardhi kwa wazee, wanawake, walemavu, na watu wengine ambao wanaweza kunyanyaswa na kunyimwa umiliki wa ardhi, wasinyimwe.
Wito huo umetolewa na mkurugenzi wa urasimishaji ardhi kutoka mpango wa serikali MKURABITA BW, Stephen Lubemalila alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ikonda kilichopo kata ya Tandala wilayani Makete.
Hatua hiyo imekuja wakati wa zoezi la upimaji ardhi likianza katika kijiji hicho hii leo kwa utambuzi zaidi.
Mkurugenzi huyo amewasihi wananchi kuanza kupanga matumizi ya ardhi kabla kuanza kwa upimaji huo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Tandala ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh, Egnatio Mtawa amesema serikali ya awamu ya tano imejikita zaidi kupunguza migogoro ya ardhi.
Mh Mtawa amesema zoezi hilo lina faida kwa mmiliki kuwa na hatimiliki ya ardhi kwani mwananchi anauwezo wa kukopa mkopo kwenye taasisi za kifedha kwa kutumia hati hiyo.
Na Asukile Mwalwembe